Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) imepokea ugeni wa viongozi wa kanda na wawakilishi kutoka Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) ukiongozwa na Katibu Mtendaji wa Mfuko huo Bw. Pradeep Kurukulasuriya uliolenga kutembelea na kujionea maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa kuboresha hali ya upatikanaji huduma ya maji Tanga awamu ya tatu kupitia ufadhili wa Hatifungani ya Kijani ambapo UNCDF ni miongoni mwa wadau muhimu walioshiriki katika hatua za awali za kufanikisha mradi huo.
Katika ziara hiyo, Katibu Mtendaji na wageni walipokea taarifa ya mradi na mwenendo wa magawio kwa wawekezaji pamoja na kutembelea eneo la mradi na kujionea kasi ya utekelezaji wa shuguli mbalimbali zinazolenga kuongeza na kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji ya uhakika kwa wakazi wa maeneo ya kihuduma ya Tanga UWASA unaotarajiwa kukamilika mapema mwezi Agosti, 2026.
Katibu Mtendaji pamoja na wageni walipata pia fursa ya kufanya kikao na sehemu ya wanufaika wa mradi wa Hatifungani katika Hospiali ya Jiji iliyopo kata ya Masiwani ambapo awali walikuwa wakipata changamoto katika kutoa huduma kutokana na adha ya upatikanaji wa huduma ya maji ya uhakika na kupitia mradi wa Hatifungani wameboreshewa miundombinu hivyo kuimarisha upatikanaji wa uhakika wa huduma ya majisafi.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Katibu Mtendaji wa UNCDF Bw. Pradeep Kurukulasuriya ameipongeza Tanga UWASA kwa uthubutu huo na kwa maendeleo mazuri ya utekelezaji wa mradi lengwa sambamba na kuonesha nia ya kuongeza wigo wa kuendelea kushirikiana.
” Tunajivunia kuwa sehemu ya mchango katika kufanikisha Hatifungani ya Kijani ya Tanga na matarajio yetu ni kwamba mradi huu utaboresha maisha ya jamii na kupitia hili Tanga UWASA imedhihirisha kuwa inawezekana kuhamasisha uwekezaji ndani ya nchi kwani takriban asilimia 65 ya uwekezaji ulitoka kwa wawekezaji wa Kitanzania, na kwa kupitia mpango huu, tumedhihirisha kuwa mitaji ya ndani inaweza kuhamasishwa ili kufadhili miradi muhimu ya maendeleo na kwa sasa tunasoma mfano huu kwa karibu, tunatafuta kuelewa ni nini kilifanya kazi vizuri, changamoto zipi zilizojitokeza, na ni somo gani tunaweza kujifunza ili tuweze kuiga mafanikio ya Hatifungani ya Tanga si tu ndani ya Tanzania bali katika nchi nyingine pia”, alisema Bw. Kurukulasuriya.
Awali kabla ya ziara hiyo, Katibu Mtendaji wa UNCDF na wageni wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Tanga UWASA, Eng. Salum Ngumbi walifika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kutoa salamu na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mhe. Dadi Kolimba aliyetoa salamu za Mkoa kwa niaba ya Mhe. Balozi Dkt. Batilda Salha Buriani Mkuu wa Mkoa wa Tanga







