Wekundu wa Msimbazi, Simba SC wameibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, mzunguko wa 28 uliopigwa leo Juni 24, 2026 mkoani Morogoro.
Simba ilianza kwa kasi na kupata bao la kwanza kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Rushine de Reuck baada ya Shomari Kapombe kuangushwa ndani ya eneo la hatari.
Kipindi cha pili Simba ilirejea uwanjani kwa kasi zaidi na kuongeza bao la pili kupitia Seleman Mwalimu aliyeingia akitokea benchi. Baadaye, Anicet Oura alifunga bao la tatu kwa shuti kali la mbali lililomshinda kipa wa Mtibwa Sugar na kutinga wavuni.
Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo, mabingwa watetezi Young Africans SC wameendeleza ubabe wao baada ya kuifunga Azam FC mabao 3-0 katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Mabao ya Yanga yalifungwa na Ibrahim Hamad “Bacca” dakika ya 41, Laurindo Aurelio “Depu” kwa penalti dakika ya 72, na Pacôme Zouzoua dakika ya 80.
Mechi hiyo ilikuwa na ushindani mkubwa na mvuto wa hali ya juu kutokana na upinzani mkali kati ya timu hizo, ikiendeleza msisimko wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Michezo mingine iliyopigwa ni pamoja na: Dodoma Jiji 0-0 JKT Tanzania, TRA United 1-1 Coastal Union, Fountain Gate 0-1 Mashujaa FC, Pamba Jiji 0-2 Mbeya City, Singida BS 3-1 Tanzania Prisons, na KMC 2-3 Namungo FC.
