Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki nchini Tanzania (EALA),James Ole Millya akizungumza kwenye bunge hilo jijini Arusha
………..
Na Happy Lazaro, Arusha
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki nchini Tanzania (EALA),James Ole Millya, amepongeza hatua zinazoendelea kuchukuliwa na serikali za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika kutekeleza mapendekezo ya ukaguzi wa hesabu kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za Jumuiya.
Akichangia mjadala bungeni, Millya amesema kuwa ushirikiano unaoendelea kati ya nchi wanachama ni ishara ya dhamira ya kuhakikisha taasisi za EAC zinafanya kazi kwa ufanisi na kwa kuzingatia misingi ya uwazi katika matumizi ya fedha za umma.
Amesema taarifa iliyowasilishwa na Waziri anayesimamia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inaonesha hatua nzuri zinazochukuliwa na serikali katika kufanyia kazi hoja na mapendekezo yanayotolewa na wakaguzi wa hesabu kila mwaka.
Millya amesisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa fedha ni muhimu katika kulinda rasilimali za Jumuiya na kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo zinawanufaisha wananchi wa Afrika Mashariki kama ilivyokusudiwa.
Aidha, ameeleza kuwa uwazi na uwajibikaji vinapaswa kuendelea kuwa sehemu ya utamaduni wa taasisi zote za EAC ili kujenga imani kwa wananchi na wadau wanaochangia maendeleo ya Jumuiya hiyo.
Millya ametoa wito kwa taasisi za EAC kuongeza kasi ya utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi na kuimarisha mifumo ya ndani ya usimamizi wa fedha ili kuondoa dosari zinazojirudia katika matumizi ya rasilimali za umma.
Amehitikisha kwa kusema kuwa utekelezaji wa mapendekezo hayo utaimarisha utendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuongeza ufanisi wa taasisi zake na kuhakikisha wananchi wa ukanda huo wanapata manufaa ya moja kwa moja kutokana na uwekezaji na programu mbalimbali zinazotekelezwa na EAC.
