Na Mwandishi wetu, Simanjiro 

MKUU wa Mkoa wa Manyara, Queen Cuthbert Sendiga amezindua basi jipya la Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, ukumbi wa mikutano na kuipongeza kwa kupata hati safi ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025.

RC Sendiga akizungumza mji mdogo wa Orkesumet, wakati wa uzinduzi huo ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Simanjiro kwa ununuzi wa basi hilo aina ya Marcopolo Tata.

“Nawapongeza mno kwa hatua hii ya ununuzi wa basi lenu hili zuri kwani ni halmashauri ya kwanza ya wilaya katika mkoa wa Manyara kununua basi, haya ni maendeleo mazuri mno,” amesema RC Sendiga.

Ameeleza kwamba tija ya basi hilo siyo kuwashwa tuu, ni kutumika kutoa huduma na kuwahi kazini kwa watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro.

“Nimefurahishwa pia na samani mpya za ukumbi wa halmashauri ambazo zitawezesha madiwani na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro kufanya kazi kwa urahisi,” amesema RC Sendiga.

Hata hivyo, ameipongeza halmashauri ya wilaya hiyo kwa kupata hati safi ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025.

Amesema changamoto zilizopo kwenye hoja 14 zilizobakia zifanyiwe kazi na kufutwa kwani hoja nyingine 26 kati ya 40 ziliweza kufanyiwa kazi na kufutwa.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Gracian Max Makota amesema gharama za kununua basi hilo ni shilingi milioni 180 kupitia mapato ya ndani.

Makota ameeleza kwamba gharama za kununua samani za ukumbi huo mpya zimetumika shilingi milioni 206 fedha kutoka serikali kuu.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Kaleya Melita Mollel amesema wamejipanga kuhakikisha wanalitunza vyema basi hilo ili litoe huduma ya usafiri ipasavyo na kwa muda mrefu.