Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) liko katika hatua za mwisho za kukamilisha ujenzi wa hospitali yenye hadhi sawa na Hospitali ya Taifa Muhimbili inayojengwa katika eneo la Msalato, jijini Dodoma.

Kauli hiyo imetolewa na Mnadhimu Mkuu wa JWTZ Luteni Jenerali Salum Haji Othman mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) wakati kamati hiyo ilipotembelea hospitali hiyo kwa lengo la kujionea maendeleo ya ujenzi wa mradi huo mkubwa wa afya.

Luteni Jenerali Othman amesema hospitali hiyo itakuwa na miundombinu ya kisasa pamoja na uwezo wa kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, hatua ambayo itasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wanajeshi na wananchi kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU),Mheshimiwa Paschal Inyasi Chinyele, amepongeza maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo na kueleza kuwa mradi huo ni muhimu kwa kuimarisha huduma za afya nchini.

Amesema kukamilika kwa hospitali hiyo kutasaidia kuongeza uwezo wa taifa katika utoaji wa huduma za matibabu ya kibingwa na kupunguza mzigo kwa hospitali nyingine za rufaa.

Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mheshimiwa Rhimo Nyansaho ameihakikishia kamati hiyo kuwa Serikali imeshalipa fedha zote zinazohitajika ili kukamilisha ujenzi huo, hatua inayotarajiwa kuharakisha ukamilishaji wa mradi huo muhimu wa kimkakati.

Aidha, Kamati hiyo imeeleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo na kuitaka JWTZ kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilika kwa wakati ili hospitali hiyo ianze kutoa huduma kwa wananchi na wanajeshi kama ilivyokusudiwa.

Hospitali hiyo inatarajiwa kuwa miongoni mwa vituo vikubwa vya matibabu nchini na kuchangia kwa kiasi kikubwa kuboresha sekta ya afya katika Jiji la Dodoma na maeneo mengine ya nchi.