Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Rosemary Senyamule, amezindua rasmi ofisi na kampuni ya Landmax Real Estate Company Limited iliyopo jijini Dodoma, katika hafla iliyofanyika Juni 24, 2026, ikiwa na kaulimbiu ya “Tunatimiza ndoto zako za umiliki wa ardhi na makazi bora.”
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, RC Senyamule amesema kuwa ardhi ya Dodoma ni utajiri mkubwa unaoendelea kuongezeka thamani kutokana na kasi ya ukuaji wa jiji hilo na ongezeko la watu pamoja na wawekezaji wanaohamia katika Makao Makuu ya Nchi.
Amesema kuwa tofauti na maeneo mengine ambako thamani ya ardhi hubaki ile ile kwa miaka mingi, Dodoma imeendelea kushuhudia ongezeko la haraka la thamani ya ardhi kutokana na mahitaji makubwa ya makazi na uwekezaji.
Aidha, amebainisha kuwa uwekezaji uliofanywa na Landmax Real Estate Company Limited ni hatua sahihi inayokwenda sambamba na juhudi za maendeleo ya Jiji la Dodoma.
Pia ameongeza kuwa ardhi iliyopo Dodoma si rasilimali ya kudumu kwani kadri mahitaji yanavyoongezeka ndivyo thamani yake inavyozidi kupanda, hivyo wananchi wanapaswa kuitumia fursa hiyo kwa manufaa yao.
RC Senyamule amesema serikali ina wajibu wa kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha huduma zinazohusiana na ardhi, vibali vya ujenzi na umilikishaji wa maeneo zinatolewa kwa wakati ili kuepusha ucheleweshaji unaoweza kusababisha wananchi au wawekezaji kuvunja sheria kutokana na kucheleweshewa huduma.
Aidha, ametoa wito kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na halmashauri nyingine za mkoa huo kuhakikisha zinaendana na kasi ya maendeleo ya wananchi na wawekezaji kwa kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali zinazohusiana na sekta ya ardhi.
Amesema kuwa serikali inapaswa kuzitambua kampuni zinazojihusisha na biashara ya ardhi na mali isiyohamishika ili kurahisisha ushirikiano katika uwekezaji na mipango ya maendeleo ya jiji.
Aidha, RC Senyamule amepongeza Landmax kwa kujipambanua kwa misingi ya uwaminifu, akisema sifa hiyo ni muhimu katika kujenga imani kwa wananchi na kuondoa changamoto zinazotokana na udanganyifu katika biashara za ardhi.
Awali, Mkurugenzi wa Landmax Real Estate Company Limited na Mbunge wa Jimbo la Mbozi, Mhe. Onesmo Mnkondya, amesema kampuni hiyo imeanzishwa kwa dhamira ya kuwa daraja kati ya ndoto za watu na mafanikio yao katika sekta ya ardhi, mali isiyohamishika na uwekezaji.
Amesema kuwa ardhi ni rasilimali muhimu inayotumika kwa makazi, biashara na maendeleo ya jamii, huku wananchi wengi wakikumbana na changamoto za kupata ardhi salama na huduma sahihi za uwekezaji.
Aidha, amebainisha kuwa Landmax inatoa huduma mbalimbali ikiwemo uuzaji na ununuzi wa ardhi na mali isiyohamishika, ushauri wa uwekezaji wa ardhi, usimamizi wa mali, urasimishaji wa nyaraka za ardhi, uendelezaji wa miradi, tafiti za soko pamoja na ushirikiano katika miradi ya maendeleo.
Ameongeza kuwa maono ya kampuni hiyo ni kuwa miongoni mwa kampuni zinazoongoza nchini katika sekta ya ardhi na mali isiyohamishika kwa kutoa huduma bora zinazozingatia uaminifu, ubunifu na uwajibikaji.
Kwa upande wake, Balozi wa kampuni hiyo na Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Mhe. Clayton Revocatus Chipando maarufu Baba Levo, amesema uwepo wa kampuni kama Landmax utasaidia kupunguza matukio ya wananchi kutapeliwa katika biashara za ardhi na mali isiyohamishika.
Amesema kuwa wananchi wanaweza kutumia kampuni hiyo kupata huduma mbalimbali ikiwemo kununua, kuuza na kupangisha nyumba au viwanja kwa kuzingatia taratibu sahihi za kisheria.
Aidha, amewataka madalali wa ardhi kushirikiana na kampuni hiyo ili kuhakikisha miamala yote inafanyika kwa uwazi na usalama, huku nyaraka zote zikihakikiwa ili kuondoa migogoro na vitendo vya utapeli.

