Paris, Ufaransa – Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa, Mheshimiwa Saidi Othman Yakubu, leo amepokea ugeni wa Mheshimiwa Sheikh Salem bin Khaled Al Qassimi, Waziri wa Utamaduni wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Elimu, Utamaduni na Sayansi ya UAE, aliyefanya ziara maalum katika Ubalozi wa Tanzania jijini Paris.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao walijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na UAE, hususan katika sekta za utamaduni, elimu, sayansi, urithi wa dunia, ubunifu na diplomasia ya kimataifa kupitia taasisi za kimataifa zikiwemo UNESCO.
Mheshimiwa Balozi Yakubu alieleza kuwa Tanzania na UAE zinaendelea kufurahia mahusiano ya karibu na ya kirafiki yaliyojengwa juu ya msingi wa kuheshimiana, ushirikiano wa kiuchumi na maono ya pamoja ya maendeleo endelevu. Alisisitiza dhamira ya Tanzania ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na UAE katika nyanja za utamaduni na ubadilishanaji wa uzoefu wa kitaalamu.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Sheikh Salem bin Khaled Al Qassimi alieleza utayari wa UAE kuendeleza ushirikiano wa karibu na Tanzania katika maeneo ya elimu, utamaduni na sayansi, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia katika majukwaa ya kimataifa.
Viongozi hao walikubaliana kuendeleza mashauriano na ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za nchi hizo mbili ili kukuza mahusiano ya watu kwa watu, kuhifadhi na kutangaza urithi wa kiutamaduni, pamoja na kuimarisha mchango wa mataifa yao katika kukuza amani, maelewano na maendeleo ya kimataifa.
Ziara hiyo imekuja wakati ambapo Tanzania na UAE zinaendelea kushuhudia ukuaji mkubwa wa mahusiano ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, kufuatia juhudi za viongozi wa mataifa hayo kuimarisha ushirikiano wenye manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili.

