Brigedia Jenerali Said Hamis Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mashindano ya CDF CUP 2026 pamoja na Nuru Mbura mwakilishi wa Azam Media wakionesha nyaraka za mkataba wa kuonesha mashindano hayo Mubashara wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo katika viwanja vya Gofu vya Lugalo Juni 24, 2026.

Brigedia Jenerali Said Hamis Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mashindano ya CDF CUP 2026 akizungumza katika uzinduzi wa michuano hiyo uliofanyika kwenye viwanja vya Golf vya Lugalo jijini Dar es Salaam kushoto ni Cdr SD Lupilya  Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi na kulia ni Luteni Kanali Penina Anthony Igwe Katibu wa Kamati ya Maandalizi. 

…………

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeandaa mashindano ya Kombe la Mkuu wa Majeshi (CDF Cup) mwaka 2026, huku likieleza kuwa mashindano hayo yanalenga kuimarisha umoja, mshikamano, afya, nidhamu na mahusiano mema kati ya jeshi na jamii inayolizunguka.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo uliofanyika katika Klabu ya Gofu ya JWTZ Lugalo jijini Dar es Salaam Juni 24, 2026, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya CDF Cup 2026, Brigedia Jenerali Said Hamis, amesema mashindano hayo yatafanyika kuanzia Julai 6 hadi 17, 2026 jijini Dar es Salaam yakiwa ni msimu wa nane tangu kuanzishwa kwake.

Brigedia Jenerali Hamis amesema kauli mbiu ya mashindano hayo ni “Amani, Umoja na Mshikamano kwa Ujenzi wa Taifa Letu”, ambayo inaakisi dhamira ya JWTZ kutumia michezo kama nyenzo ya kujenga mahusiano, uzalendo na ushirikiano miongoni mwa wanajeshi na wananchi.

Amesema madhumuni ya mashindano hayo ni kuimarisha utimamu wa mwili na afya ya akili kwa maafisa na wapiganaji, kujenga ujasiri, ukakamavu na kujiamini, pamoja na kubaini na kukuza vipaji vya wanamichezo ndani ya jeshi.

Ameeleza kuwa mashindano hayo yatahusisha timu kutoka katika makamandi mbalimbali ya JWTZ ikiwemo Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, Jeshi la Anga, Jeshi la Wanamaji, Makao Makuu ya Jeshi, Jeshi la Akiba na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Brigedia Jenerali Hamis amesema jumla ya michezo 13 itashindaniwa katika mashindano hayo ikiwemo mpira wa miguu, netiboli, mpira wa wavu, mpira wa mikono, mpira wa kikapu, riadha, kulenga shabaha, kuogelea, kupita kwenye vikwazo, darts, soka la ufukweni na michezo mingine, huku mchezo mpya wa pool table ukiwa umeongezwa mwaka huu.

Aidha, amesema mchezo wa ngumi utakuwa na upekee katika CDF Cup ya mwaka huu ambapo mabondia kutoka makamandi mbalimbali watashindania mikanda maalum ya CDF Cup kwa uzito tofauti kwa wanaume na wanawake, ikiwa ni sehemu ya kutambua vipaji vya wanajeshi katika mchezo huo.

Amesema wananchi watapata fursa ya kushuhudia mashindano hayo bila kiingilio katika viwanja mbalimbali jijini Dar es Salaam ikiwemo Azam Complex Chamazi ambako kutafanyika ufunguzi na ufungaji wa mashindano hayo, pamoja na viwanja vya kambi mbalimbali za jeshi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Benki ya Azania, Yahaya Mbanka, amesema benki hiyo imeona umuhimu wa kushirikiana na JWTZ katika kudhamini mashindano hayo kwa kuwa michezo ni chombo muhimu cha kujenga afya, nidhamu, uzalendo na mshikamano.

Yahaya Mbanka amesema Benki ya Azania inashiriki kudhamini CDF Cup kwa mara ya kwanza mwaka huu na imekabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Sh milioni 200 kusaidia kufanikisha mashindano hayo.

Naye Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi Benki ya NMB, Aikansia Muro, amesema benki hiyo imeendelea kuwa mshirika wa karibu wa JWTZ katika shughuli mbalimbali na mwaka huu imeunga mkono mashindano hayo kwa kukabidhi vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh milioni 150.

Amesema NMB inaamini vifaa hivyo vitachangia kuongeza ushindani na ubora wa mashindano hayo, huku akipongeza uongozi wa JWTZ kwa kuendelea kuendeleza michezo ndani ya jeshi.

Kwa upande wa Benki ya CRDB, Meneja wa Wateja Binafsi, Farida Mbwana, amesema benki hiyo imekuwa mdhamini wa michezo mbalimbali nchini na itaendelea kushirikiana na JWTZ katika kuendeleza michezo na kuimarisha amani, umoja na mshikamano katika jamii.