23 Juni 2026

Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Mhe. Enock Koola, ameishauri Serikali kuweka dhamana kwa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU) ili kuwezesha ulipaji wa madeni ya zaidi ya miaka 10 yanayodaiwa na vyama vya msingi vya ushirika, hatua ambayo amesema itasaidia kurejesha imani ya wakulima na kuimarisha mfumo wa ushirika katika mkoa huo.

Mhe. Koola ametoa rai hiyo leo Jumanne, Juni 23, 2026 bungeni wakati wa kipindi cha maswali na majibu alipouliza swali kwa Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali kufufua zao la kahawa na kuimarisha maslahi ya wakulima wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Mbunge huyo amesema baadhi ya vyama vya msingi vya ushirika katika maeneo ya Moshi Vijijini na Vunjo vinadai zaidi ya Shilingi milioni 800 kutoka KNCU tangu mwaka 2011, hali ambayo imeendelea kudhoofisha imani ya wanachama na wakulima kwa vyama vyao.

“Je, Serikali iko tayari kutoa dhamana ili wakulima hao waweze kulipwa fedha zao na kurejesha imani kwa vyama vya msingi kuendelea kufanya kazi?” alihoji Mhe. Koola.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, amesema tayari amezungumza na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika na kumuelekeza kwenda Mkoa wa Kilimanjaro kukutana na viongozi wa vyama vya msingi pamoja na KNCU ili kutafuta suluhisho la haraka la mgogoro huo wa muda mrefu.

Mhe. Silinde amesema Serikali inatafuta njia bora za kuhakikisha wakulima wanalipwa madeni yao, ikiwemo kuangalia uwezekano wa kuweka dhamana itakayosaidia kufanikisha malipo hayo.

“Kuhusu deni la KNCU, nimeshazungumza na Mrajisi wa Ushirika na nimemuelekeza kwenda Kilimanjaro akakutane na vyama vya msingi pamoja na KNCU ili kutafuta suluhisho la haraka, ikiwemo kuona namna bora ya Serikali kuweka dhamana kwa wakulima hao kulipwa madeni yao,” alisema Mhe. Silinde.

Katika swali lake la pili la nyongeza, Mhe. Koola alitaka kufahamu iwapo maelekezo ya Waziri wa Kilimo ya kutotoa leseni kwa wadau wanaodaiwa na wakulima yataihusu pia KNCU, ambayo bado inakabiliwa na madai kutoka kwa baadhi ya vyama vya msingi.

Akijibu hoja hiyo, Mhe. Silinde amesema maelekezo ya Waziri wa Kilimo kuhusu utoaji wa leseni bado yapo, lakini akasisitiza kuwa KNCU ni chama kikuu kinachomilikiwa na vyama vya msingi, hivyo wanachama wenyewe wana nafasi ya kuamua namna ya kutekeleza maelekezo hayo kwa kuzingatia maslahi ya ushirika wao.

Awali, akijibu swali la msingi, Mhe. Silinde amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kufufua zao la kahawa katika Mkoa wa Kilimanjaro baada ya uzalishaji kushuka kutoka wastani wa tani 25,000 za kahawa safi kwa mwaka kabla ya uhuru hadi takribani tani 4,000 kwa mwaka katika miaka ya hivi karibuni.

Ametaja hatua hizo kuwa ni pamoja na uzalishaji na usambazaji wa miche bora ya kahawa, maboresho ya mfumo wa masoko pamoja na kuimarisha mazingira ya biashara kwa wakulima.

Kwa mujibu wa Mhe. Silinde, maboresho hayo yamewezesha vyama vya msingi vya ushirika mkoani Kilimanjaro kupata masoko ya moja kwa moja, ikiwemo soko la Japan, ambapo mwaka 2025 kampuni ya Farmers Kilimanjaro Coffee Ltd iliuza kilo 57,600 za kahawa zenye thamani ya dola za Marekani 594,402.