Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, ameagiza kuchukuliwa hatua kwa maafisa rasilimali watu watakaobainika kusababisha watumishi wa umma kushindwa kupanda madaraja kwa uzembe licha ya kutimiza vigezo vinavyotakiwa.
Ametoa maelekezo hayo Juni 23,2026 Kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 jijini Dodoma, ambapo alimwakilisha
Prof. Shemdoe amesema kuwa wakuu wa taasisi na maafisa rasilimali watu wanapaswa kushughulikia changamoto za watumishi wanaowaongoza badala ya kuwa chanzo cha malalamiko yanayoweza kuepukika.
Aidha, amebainisha kuwa baadhi ya maafisa rasilimali watu wamekuwa wakisababisha ucheleweshaji wa upandishaji madaraja kutokana na kushindwa kutekeleza wajibu wao kwa wakati katika mifumo ya kiutumishi.
Ameongeza kuwa hata yeye aliwahi kukumbwa na changamoto ya kucheleweshewa kupanda cheo kwa mwaka mmoja kutokana na kutokukamilishwa kwa taratibu muhimu za kiutumishi na afisa husika.
Pia ameelekeza kufanyika tathmini kwa maafisa rasilimali watu wakuu waliosababisha watumishi kushindwa kupanda madaraja katika mwaka wa fedha 2025/2026 ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao.
Amesema kuwa watumishi wanaotimiza vigezo vya kupandishwa madaraja hawapaswi kunyimwa haki hiyo kwa sababu ya uzembe wa mtu mmoja.
Aidha, amewataka waajiri wote kutenga fedha za ushiriki katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma na kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma bora kupitia maonesho hayo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR-MUUUB), Bw. Juma Mkomi, amesema maadhimisho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa azimio la Umoja wa Afrika la kuadhimisha Siku ya Utumishi wa Umma Barani Afrika.
Amesema kuwa maadhimisho hayo yanalenga kutambua mchango wa watumishi wa umma katika maendeleo ya taifa, kuhamasisha ubunifu katika utoaji wa huduma na kupata mrejesho kutoka kwa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi za umma.

