Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki nchini Tanzania ,Machano Aly Machano akizungumza na waandishi  wa habari mara baada ya bunge hilo
………….
Na Happy Lazaro, Arusha 
Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki limeanza rasmi kikao chake cha bajeti mjini Arusha, ambapo wabunge kutoka nchi wanachama wanatarajiwa kujadili masuala mbalimbali yenye lengo la kuimarisha maendeleo ya jumuiya hiyo.
Akizungumza mjini Arusha, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki nchini Tanzania ,Machano Aly Machano amesema ana matumaini makubwa kuwa vikao hivyo vitazaa maamuzi yatakayochochea maendeleo ya jumuiya huku wabunge wakiendelea kutekeleza majukumu yao katika mazingira mazuri ya kazi.
“Kabla ya kuanza kwa vikao vya bunge, shughuli za kamati mbalimbali zilifanyika na kuwasilisha ripoti zake, ambazo sasa zimeanza kujadiliwa katika kikao cha bunge. “amesema Machano.
Wabunge wanatarajia pia kupokea na kujadili taarifa ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema kuwa kikao hicho cha bajeti kinahusisha kupitia na kuidhinisha matumizi ya taasisi mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo Bunge la Afrika Mashariki, Mahakama ya Afrika Mashariki, Sekretarieti ya Jumuiya pamoja na taasisi nyingine zilizo chini ya jumuiya hiyo.
“Katika siku ya kwanza ya kikao hicho, ripoti ya Kamati ya Hesabu za Fedha iliwasilishwa na kujadiliwa, huku wajumbe wakijadili kwa kina masuala yanayohusu matumizi bora na usimamizi wa fedha za jumuiya.”amesema Machano .
Aidha, mjadala umeendelea katika Kamati ya Mawasiliano, Biashara na Utalii, ambapo wajumbe wamejadili changamoto zinazokabili maeneo ya mipakani kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na urahisishaji wa usafirishaji wa watu na bidhaa katika mipaka ya Tanzania, Kenya, Uganda na nchi nyingine wanachama ili kuimarisha biashara na ushirikiano wa kikanda.
Kamati hiyo imewasilisha mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuondoa vikwazo vinavyokwamisha shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo ya mipakani.
Wabunge wanatarajia kupitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, hatua ambayo itatoa mwongozo na rasilimali za kutosha kwa jumuiya kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Mkataba wa Kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa upande wake Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) kutoka Jamhuri ya Sudan Kusini, Dkt. Woda Jago, amesema ameridhishwa na kurejea kwa vikao vya bunge hilo baada ya kusimama kwa muda mrefu tangu Novemba mwaka jana.
Akizungumza baada ya kikao cha bunge, Dkt. Woda amesema wajumbe wote wamejitokeza kushiriki kikao hicho, huku pia akiwakaribisha wajumbe wapya kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Shirikisho la Somalia.
Aidha, Dkt. Woda amewapongeza baadhi ya wajumbe wa bunge hilo walioteuliwa kushika nyadhifa za Naibu Waziri katika nchi zao, akiwemo Mheshimiwa James Ole akisema uteuzi huo utaimarisha ushirikiano kati ya bunge na serikali za nchi wanachama.
Kwa mujibu wa Dkt. Woda amesema  hatua hiyo itasaidia kulifufua bunge hilo na kuliwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
Katika kikao hicho, wabunge walijadili ripoti mbili muhimu. Ripoti ya kwanza ilikuwa ya Kamati ya Hesabu za Serikali iliyohusu ukaguzi wa hesabu za mwaka wa fedha 2022/2023 pamoja na 2021/2022, mjadala ambao ulikuwa umeahirishwa kutoka kikao kilichopita.
Ripoti ya pili ilitoka Kamati ya Mawasiliano, Biashara na Uwekezaji (CTI), ikijikita katika masuala ya wafanyabiashara wa mipakani na changamoto wanazokabiliana nazo katika shughuli zao za kila siku.
Dkt. Woda  amesema mijadala hiyo ilikuwa muhimu kwa maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na ustawi wa wananchi wa nchi wanachama.
Ameongeza kuwa pamoja na umuhimu wa ripoti hizo, wabunge walitarajia kujadili bajeti ya jumuiya hiyo katika kikao kitakachofanyika kesho.
Kwa ujumla, amesema kikao hicho kimeweka msingi mzuri wa kuendeleza shughuli za bunge na kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika Afrika Mashariki.