Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani imeongeza makusanyo ya mapato kutoka Sh bilioni 27 mwaka 2015/2016 hadi Sh bilioni 266 mwaka 2025/2026, mafanikio yanayoakisi kuimarika kwa shughuli za kiuchumi na mwitikio wa walipa kodi.

Akizungumza Julai 23,2026 katika kongamano la wadau na walipa kodi kuelekea maadhimisho ya miaka 30 ya TRA tangu kuanzishwa kwake, Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani, Peter Eliona, alisema ongezeko hilo limetokana na ushirikiano wa walipa kodi pamoja na maboresho ya mifumo ya ukusanyaji mapato.

Alieleza mwaka 2015/2016 TRA Pwani iliweka lengo la kukusanya Sh bilioni 23 lakini ilifanikia Sh bilioni 27, huku mwaka 2025/2026 lengo likiwa Sh bilioni 235 na makusanyo kufikia Sh bilioni 266.

Alieleza kuwa mapato yanayokusanywa yanawezesha Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi katika sekta mbalimbali.

Hata hivyo, Eliona alifafanua TRA inaendelea kukabiliana na changamoto ya wafanyabiashara wa magendo, hususan wa spirit na vileo, wanaotumia stempu feki ili kulipa kiwango kidogo cha kodi, hali inayosababisha upotevu wa mapato ya Serikali.

Aliongeza kuwa mamlaka hiyo pia inakabiliana na mabadiliko ya teknolojia yanayochochea ongezeko la biashara zinazofanyika kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali, ili kuhakikisha mapato yote stahiki yanakusanywa.

Vilevile aliwasihi wafanyabiashara kukamilisha malipo yao ya kodi kwa wakati ili kuepuka adhabu, penati na usumbufu unaoweza kujitokeza kutokana na kuchelewesha malipo.

Kwa upande mwingine, alisema TRA imeendelea kuboresha mifumo yake ya kielektroniki, hatua iliyorahisisha upatikanaji wa huduma kwa walipa kodi na kuongeza uwazi katika shughuli za ukusanyaji mapato.

Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Pwani, Said Mfinanga, alipongeza mageuzi yanayofanywa na TRA, akisema matumizi ya mifumo ya kidijitali yamepunguza muda na gharama za kufuata huduma za kodi.

Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Pwani, Abdallah Ndauka, aliishauri TRA kuendelea kushirikiana kwa karibu na wafanyabiashara ili kuwajengea uelewa wa masuala ya kodi na kukuza biashara zao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wamachinga Mkoa wa Pwani, Philemon Maliga, aliomba kuongezwa kwa elimu ya mlipa kodi kwa kundi hilo ili kuongeza uelewa na ushirikiano kati yao na mamlaka hiyo.

Mwenyekiti wa Chama cha Maofisa Usafirishaji Kibaha, Saleh Jamal, alisema madereva wa bodaboda wana mchango mkubwa katika ukuaji wa shughuli za kiuchumi, akibainisha kuwa kwa sasa idadi yao imefikia 7,700 na wanahitaji kuendelea kupewa elimu ya kodi.

TRA ilianzishwa kwa Sheria Na. 11 ya mwaka 1995 na kuanza rasmi shughuli zake za ukusanyaji mapato Julai 1, 1996, ikiwa na jukumu la kusimamia na kukusanya kodi pamoja na mapato mengine ya Serikali Kuu.