Same, Kilimanjaro — Huku wakisubiri kuwasili kwa Mwenge wa Uhuru Juni 28 mwaka huu, wananchi wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wamesema ujio huo unatarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi na kuongeza fursa za biashara kwa makundi mbalimbali ya jamii.
Kijana anayejishughulisha na usafiri wa bodaboda katika Stendi ya Same Mjini, John Mzava, alisema ujio wa Mwenge wa Uhuru huambatana na ongezeko la wageni na shughuli mbalimbali zinazowanufaisha wananchi kiuchumi.
“Sisi vijana wa bodaboda tunajiandaa kwa hamu. Mwenge ukifika huja na watu wengi, hivyo abiria wanaongezeka na kipato chetu kinapanda. Hii ni fursa muhimu kwetu kujiongezea kipato,” alisema Mzava.
Naye mama lishe anayefanya biashara katika Soko Kuu la Same, bi Zaina Ishima , alisema tayari wameanza kufanya maandalizi ya kuongeza bidhaa ili kukidhi mahitaji ya wageni watakaohudhuria shughuli za Mwenge wa Uhuru.
“Kila Mwenge unapofika mauzo ya chai, maandazi na vyakula mbalimbali huongezeka. Wageni wanahitaji huduma na sisi wafanyabiashara tunapata nafasi ya kuongeza mapato yetu,” alisema.
Baadhi ya wananchi walisema mbali na kuhamasisha biashara, Mwenge wa Uhuru unaendelea kuwa chombo muhimu cha kuhimiza uzalendo, amani na ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo.
Vijana kadhaa walieleza kuwa ujumbe unaobebwa na Mwenge wa Uhuru huwapa hamasa ya kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali, kujitolea katika shughuli za kijamii na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii zao.
Viongozi wa Wilaya ya Same wamesema maandalizi ya kuupokea Mwenge wa Uhuru kutoka Mkoa wa Tanga yamekamilika, huku ukitarajiwa kuzindua, kukagua na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya maji, afya, elimu na miundombinu ya barabara kabla ya kuendelea na ziara yake katika wilaya nyingine za Mkoa wa Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa ratiba ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu, Mwenge utaingia Mkoa wa Kilimanjaro kupitia Wilaya ya Same Juni 28, ukiendelea kusambaza ujumbe wa Tanzania ni Yetu Sote tushikamane Kwa pamoja kuleta Maendeleo
Wakazi wengi wa Same wamesema wanasubiri kwa hamu ujio huo, wakiamini kuwa mbali na kuimarisha mshikamano wa kitaifa, Mwenge wa Uhuru ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika jamii.

