Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla  akizungumza katika ziara hiyo jijini Arusha leo.
………..
Na Happy Lazaro, Arusha 
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla  amekagua mradi wa usimikaji taa kwenye Uwanja wa ndege wa Arusha pamoja na ujenzi wa barabara ya Mbauda- Tanganyika Packers- Losinyai, akiagiza kasi katika utekelezaji wa miradi hiyo ili iweze kukamilika kabla ya ratiba za Mkutano wa Jumuiya ya Mabunge duniani (IPU) na michuano ya AFCON itakayochezwa 2027.
Akiwa katika uwanja wa ndege Arusha, Mhe. Makalla ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo, akisema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya shilingi Bilioni 11 kutekeleza mradi huo, matamanio yake yakiwa ni kuona uwanja huo unatumika usiku na mchana ili kuchochea shughuli za Utalii, akisema ni matarajio yake kuwa mradi huo utakabidhiwa Agosti Mosi, kwani vifaa vyote vinavyohitajika vitaanza kuingia Mkoani hapa kuanzia kesho Jumanne.
Aidha akikagua ujenzi wa barabara, Mhe. Makalla licha ya kueleza kuridhishwa na kazi inayoendelea, amesisitiza umuhimu wa Taasisi na Mashirika ya Umma kumsaidia Mkandarasi kuweza kutekeleza wajibu wake, akitaka kuondolewa haraka kwa miundombinu ya Tanesco na Idara za Maji, kwani imekuwa kikwazo kwa Mkandarasi wa mradi huo.
“Tanesco waondoe nguzo zilizopo kwenye mradi huu hivyo hivyo kwa Mamlaka za Maji nazo ziondoe miundombinu yao iliyo kwenye maeneo ya ujenzi wa barabara ili kutoa nafasi ya kutekelezwa mradi huu kwa wakati. Malipo ya awali yameshalipwa na nitumie nufsa hii kumshukuru sana Rais Samia kwa uwekezaji wake huu mkubwa na miundombinu hii inalenga pia kutupunguzia foleni katika Jiji la Arusha kuelekea kwenye michuano ya AFCON 2027.” amesema Mhe. Makalla.
Kwa upande wake Mkandarasi Mkazi wa Kampuni ya China Civil Engineering Construction Company Bw. Liu Nanjing, amemuahidi Mhe. Makalla kukamilisha barabara hiyo kwa wakati, akieleza pia mkakati wao wa kuendelea kutoa fursa nyingi zaidi za ajira kwa Vijana wa Mkoa wa Arusha katika utekelezaji wa barabara hiyo yenye jumla ya urefu wa Kilomita 70.