Na Oscar Assenga,TANGA.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, amepongeza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya kuboresha upatikanaji wa maji safi katika eneo la Mzizima hadi Mikocheni, akisema unadhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi.

Mwenge wa Uhuru 2026 umetembelea na kukagua mradi huo unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) katika Kata ya Mzizima, ambapo viongozi wa mbio hizo walieleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wake.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo na kushiriki katika zoezi la kumuunganishia mteja mpya huduma ya maji safi, Mwang’onda alisema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza mkakati wa kuboresha huduma za maji nchini ili kumtua mama ndoo kichwani.

Alisema dhamira hiyo inaonekana kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa katika sekta ya maji nchini, huku akiipongeza Tanga UWASA kwa usimamizi mzuri wa mradi huo ambao unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi, Mhandisi Aaron Chanimbaga, akisoma taarifa ya utekelezaji alisema mradi huo wenye thamani ya Shilingi milioni 233.4 umefikia asilimia 50 ya utekelezaji.

Alieleza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba mwaka huu na unalenga kunufaisha zaidi ya wananchi 4,780 kwa kuwapatia huduma ya maji safi na salama kwa uhakika.

Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 zinaongozwa na kauli mbiu isemayo: “Tanzania ni yetu sote, tushirikiane kwa pamoja kuleta maendeleo.”