Mabigwa Watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga SC imerejesha kileleni mwa Ligi Kuu Bara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate katika mchezo uliochezwa leo Juni 18, 2026 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Mabao ya haraka yaliyofungwa na kiungo Pacome Zouzoua dakika ya 52 na mshambuliaji Laurindo Dilson Maria ‘Depu’ dakika ya 54 yaliihakikishia Yanga ushindi muhimu uliowarejesha kileleni, huku Simba ikishuka nafasi ya pili baada ya kukaa juu kwa muda mfupi.

Kabla ya mchezo huo, Simba ilikuwa imepanda kileleni kwa muda baada ya kuifunga Mbeya City bao 1-0 na kufikisha pointi 64. Hata hivyo, ushindi wa Yanga umeifanya kufikisha pointi 66 na kurejesha tofauti ya pointi mbili juu ya watani wao.

Bao la Pacome lilikuwa la nane kwake msimu huu wa Ligi Kuu, akivunja ukimya wa muda mrefu tangu alipofunga mabao mawili katika ushindi wa 6-0 dhidi ya Mbeya City Aprili 16, 2026.

Kwa upande wa Depu, bao hilo lilikuwa la saba katika Ligi Kuu tangu alipojiunga na Yanga dirisha dogo la usajili la Januari 2026 akitokea Radomiak Radom FC ya Poland.

Mshambuliaji huyo raia wa Angola alikuwa hajafunga tangu Machi 12, 2026, alipoiwezesha Yanga kushinda 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons.

Yanga iliingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri dhidi ya Fountain Gate baada ya kushinda mabao 2-0 katika mchezo wa raundi ya kwanza uliochezwa Desemba 4, 2025.

Nao Fountain Gate walikuwa wakisaka kisasi cha kipigo hicho, lakini walishindwa tena kupata matokeo chanya.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kuendelea kuongoza msimamo wa ligi kwa pointi 66, baada ya kushinda mechi 20, kutoka sare sita na kupoteza mchezo mmoja pekee.

Kwa upande wa Fountain Gate, imebaki nafasi ya 10 ikiwa na pointi 29, baada ya kushinda mechi nane, sare tano na kupoteza 14.