Na Mwamvua Mwinyi, Mafia

Uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka za plastiki zinazotupwa ovyo baharini umeendelea kuwa tishio kubwa kwa mifumo ya ikolojia ya bahari, viumbe wa majini na shughuli za kiuchumi zinazotegemea rasilimali hizo, ikiwemo uvuvi, utalii na kilimo cha mwani katika fukwe mbalimbali ikiwemo Mafia.

Kutokana na changamoto hiyo, Shirika la Harakati na Uwezeshaji wa Mazingira Tanzania (TEEMO) limezindua rasmi Kituo cha Ukusanyaji na Urejelezaji wa Plastiki katika eneo la Kibaoni, Kata ya Kiegeani, wilayani Mafia kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa taka za plastiki, kupunguza uchafuzi wa mazingira ya bahari na kukuza uchumi wa mzunguko (circular economy) katika jamii za visiwani.

Mradi huo unafadhiliwa na kampuni ya C-Weed Mwani kwa kushirikiana na Cargill, wadau wanaoshiriki katika juhudi za kulinda mazingira, kusaidia jamii za pwani na kuendeleza uchumi wa buluu.

Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Wilaya ya Mafia ambaye pia ni Ofisa Afya wa Wilaya, Othman Masanga, aliwashukuru wadau hao kwa mchango wao katika kuhifadhi mazingira na kuhakikisha shughuli za kiuchumi zinazotegemea bahari zinaendelea kwa manufaa ya wananchi.

Aidha, aliwataka wadau wengine kuendelea kuibuka na miradi endelevu itakayosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuifanya Mafia kuwa mfano wa utunzaji wa mazingira ya bahari.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TEEMO, Winfrida Shonde, alisema kituo hicho ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa shirika hilo wa kupambana na uchafuzi wa plastiki na kulinda mazingira ya pwani kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Alisema kituo hicho kitakuwa na jukumu la kupokea, kuchambua na kusafirisha taka za plastiki zinazokusanywa kutoka maeneo mbalimbali ya Mafia kwa ajili ya kuchakatwa na kurejelezwa, badala ya kuishia baharini au kutapakaa kwenye mazingira.

“Tunataka kuona jamii inakuwa sehemu ya suluhisho kwa kushiriki kikamilifu katika ukusanyaji na usimamizi sahihi wa taka za plastiki ili kulinda mazingira na rasilimali za bahari,” alieleza Shonde.

Kupitia mradi huo, TEEMO inalenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa usimamizi sahihi wa taka, kuhamasisha ukusanyaji wa plastiki kutoka majumbani, fukwe na maeneo ya umma pamoja na kufungua fursa za kiuchumi kupitia shughuli za urejelezaji.

Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Kombo Mzee, kijana kutoka Kata ya Kilindoni, alifafanua mradi huo ni fursa muhimu kwa vijana kushiriki katika utunzaji wa mazingira huku wakijifunza mbinu za urejelezaji wa plastiki.

“Hii ni fursa kwa vijana, hivyo tujitokeze kwa wingi kushiriki katika jitihada za kutunza mazingira na kujifunza namna bora ya kurejeleza plastiki,” alibainisha.

Mradi wa TEEMO Plastic Collection Centre – Mafia unatarajiwa kuwa mfano wa ubunifu katika usimamizi wa taka za plastiki visiwani na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi, mashirika ya kiraia na jamii katika kukabiliana na changamoto za mazingira na kukuza maendeleo endelevu.