Na Mwamvua Mwinyi, Mafia
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeendesha mafunzo ya uzingatiaji wa haki za binadamu katika ufikiaji, upatikanaji na usimamizi wa rasilimali za bahari kwa wavuvi wadogo, vikundi vya kina mama wachakataji wa samaki, Chama cha Wanawake Wavuvi Tanzania (TAWFA) pamoja na Kamati za Usimamizi wa Fukwe (BMU) wilayani Mafia.
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ofisi za Uvuvi eneo la Bondeni Pwani, kijiji cha Kilindoni, yamelenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora katika matumizi na usimamizi wa rasilimali za bahari.
Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Ofisa Uchunguzi Mkuu kutoka Tume hiyo, Jovina Mchunguzi, alisema elimu ya haki za binadamu ni jukumu la wadau wote na si Tume pekee, hivyo amewahimiza wadau kushirikiana katika kufikisha elimu hiyo kwa wananchi.
“Wadau tuungane na Tume katika kufikisha fursa hii kwa wananchi wote, sisi tupo tayari kushirikiana nao,” alieleza.
Kwa upande wake, Ofisa Uvuvi wa Kilindoni, Jedia Joseph, alisema mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza uelewa wa wananchi katika kutambua haki zao na kuleta mabadiliko chanya katika shughuli zao za kila siku.
Mada mbalimbali zilifundishwa wakati wa mafunzo hayo, ikiwemo haki zilizoainishwa katika Katiba, umuhimu wa bima za afya kwa wavuvi na wachakataji wa samaki, haki za matumizi ya rasilimali za bahari pamoja na utunzaji wa mazingira katika maeneo ya shughuli za kiuchumi.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Silima Juma, Katibu wa Kamati Ndogo ya Hifadhi kutoka kijiji cha Kiegeani, alisema mafunzo hayo yamewapa mwamko mpya wa kutambua na kutetea haki zao.

