Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Wenye Viwanda Nchini (CTI), limepongeza Bajeti Kuu ya mwaka 2026/2027 ikisema kuwa kama itatekelezwa vizuri itasaidia kulinda na kustawisha viwanda vya ndani .
Shirikisho hilo limesema serikali imechukua asilimia 50 ya mapendekezo ya wenye viwanda na kuyaweka kwenye bajeti kwani kati ya mapendekezo 110 waliyoyawasilisha, 51 yamechukuliwa.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Shirikisho hilo, Hussein Sufian wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali yaliyomo kwenye bajeti kuu ya serikali.
Alisema kwenye bajeti hiyo serikali imejitajidi kwa kiasi kikubwa kuchumua mapendekezo ya wenye viwanda kuhusu kodi mbalimbali ambazo zilikuwa kero kwa wafanyabiashara na wenye viwanda.
Alisema CTI inaona kuwa bajeti hii, yenye thamani ya Shilingi trilioni 62.5, inaendana na malengo ya kujenga uchumi stahimilivu kupitia matumizi ya teknolojia ya kidijitali, uwekezaji wa kimkakati na sera endelevu za kifedha.
Aidha, alipongeza dhamira ya Serikali ya kuongeza mapato ya ndani huku ikiendelea kuboresha mazingira ya biashara ni hatua muhimu katika kujenga uchumi unaojitegemea.
Alisema Shirikisho linafurahishwa na hatua mbalimbali zilizopendekezwa katika bajeti hiyo, ikiwemo kuimarisha mfumo wa pamoja wa ukusanyaji wa tozo na ada, kupunguza urasimu wa taasisi za udhibiti, kuboresha mifumo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kutumia teknolojia za kisasa na akili mnemba, pamoja na kuanzisha ukaguzi wa pamoja ili kupunguza usumbufu kwa wawekezaji na wenye viwanda.
“CTI inaipongeza Serikali kwa kuzingatia sehemu kubwa ya mapendekezo yaliyowasilishwa na sekta ya viwanda, hususan yale yanayolenga kulinda viwanda vya ndani, kuongeza thamani ya malighafi za ndani, kukuza ajira, kuchochea uwekezaji na kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi,” alisema.
Hata hivyo, alisema CTI imebaini kuwa baadhi ya mapendekezo yaliyomo kwenye bajeti yanaweza kuongeza gharama za uzalishaji kwa baadhi ya viwanda.
Alisema miongoni mwa maeneo hayo ni mabadiliko ya ushuru wa bidhaa (excise duty), tozo za mauzo ya nje kwa baadhi ya mazao na bidhaa zake, ushuru wa malighafi za uzalishaji wa mafuta ya kula pamoja na tozo zinazohusiana na sukari ya viwandani.
“Shirikisho linaamini kuwa maeneo haya yanahitaji kuendelea kujadiliwa ili kuhakikisha malengo ya kuongeza mapato ya Serikali hayaathiri ushindani wa viwanda vya ndani na uwezo wa bidhaa za Tanzania kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa,” alisema.
Alisema CTI inaamini kuwa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 imeweka msingi mzuri wa kuendelea kukuza uchumi wa taifa, kuimarisha mazingira ya biashara na kuongeza mchango wa sekta ya viwanda katika maendeleo ya nchi.
Alisema Shirikisho litaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine kuhakikisha sekta ya viwanda inaendelea kuwa injini muhimu ya ukuaji wa uchumi, uzalishaji wa ajira na ustawi wa wananchi.
“CTI inaishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikisha sekta binafsi katika mchakato wa kuandaa sera na bajeti, na inaahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa mikakati itakayochochea maendeleo ya viwanda na uchumi wa Tanzania kwa ujumla,” alisema.

