Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akibonyeza Kitufe kuashiria uzinduzi wa Kitabu cha miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaamtarehe 12 Juni, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar pamoja na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Bw. Emmanuel Tutuba kwenye Maadhimisho ya cha miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Juni, 2026.

…………

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameziagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na taasisi za fedha nchini kubuni mifumo rafiki ya utoaji mikopo kwa vijana, wanawake na wajasiriamali wadogo wasiokuwa na mali za kuweka dhamana, kwa kuzingatia historia yao ya uaminifu katika kurejesha mikopo.

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Juni 12, 2026 wakati akizungumza katika maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania yaliyofanyika katika Ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Amesema bado wananchi wengi wenye uwezo wa kufanya biashara na kurejesha mikopo wanakosa fursa kutokana na kutokuwa na dhamana za kawaida zinazotakiwa na taasisi za fedha, hali inayokwamisha ukuaji wa sekta binafsi na maendeleo ya wananchi.

“Mama lishe ambaye hana hati ya nyumba wala gari lakini ana historia nzuri ya biashara ya miaka mingi na marejesho mazuri ya fedha anapaswa kuaminiwa na kupewa mkopo. Uaminifu ni mali kubwa kuliko hata dhamana ya mali inayoonekana,” amesema Rais Samia.

Amesisitiza kuwa taasisi za fedha zinapaswa kutumia ubunifu wa kidijitali pamoja na taarifa za miamala ya biashara kuwajengea uwezo wananchi kuaminika badala ya kutegemea dhamana za mali pekee.

Aidha, Rais Samia amesema mfumo wa fedha nchini unatakiwa kwenda sambamba na maisha halisi ya wananchi kwa kuhakikisha huduma za kifedha zinachochea ukuaji wa biashara ndogo ndogo, kuongeza ajira na kuinua kipato cha wananchi wa kawaida.

Amesema mafanikio ya sekta ya fedha hayapaswi kupimwa kwa takwimu za ukuaji wa uchumi pekee, bali namna yanavyowagusa wananchi moja kwa moja katika shughuli zao za kila siku.

“Tusibaki kuhesabu idadi ya waliofikiwa na huduma za kifedha pekee, bali tuangalie ni wangapi wameongeza kipato, biashara ngapi zimekua na vijana wangapi wameweza kugeuza mawazo yao kuwa kampuni,” amesema.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ameitaka Benki Kuu kuendelea kusimamia mifumo ya malipo ya kidijitali ili kusaidia kuongeza uwazi wa mapato ya serikali, kupunguza ukwepaji kodi na kurahisisha huduma kwa wananchi.

Amesema matumizi ya mifumo hiyo hayapaswi kuongeza mzigo kwa wafanyabiashara wadogo bali yawasaidie kuingia rasmi katika uchumi na kushiriki kuchangia pato la taifa.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, amesema Benki Kuu ya Tanzania imekuwa nguzo muhimu ya uhuru wa kiuchumi wa taifa tangu kuanzishwa kwake mwaka 1966, huku akieleza kuwa mafanikio ya taasisi hiyo yamejengwa na misingi ya taaluma, mageuzi na usimamizi madhubuti wa sekta ya fedha.

Amesema katika kipindi cha miaka 60, BoT imeendelea kukua kutoka mfumo mdogo wa usimamizi wa fedha hadi kuwa taasisi yenye mchango mkubwa katika uthabiti wa uchumi wa taifa.

Naye Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema katika kipindi cha miaka 60 taasisi hiyo imefanikiwa kuimarisha sekta ya fedha, kudhibiti mfumuko wa bei na kuongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma za kifedha.

Amesema BoT itaendelea kuimarisha mifumo ya kisasa ya fedha, matumizi ya teknolojia ya akili unde pamoja na kuongeza usalama wa mifumo ya malipo ili kuhakikisha sekta ya fedha inaendelea kuwa salama, himilivu na jumuishi kwa wananchi wote.

Bw. Tutuba amesema mafanikio hayo yamechangiwa na mageuzi mbalimbali yaliyofanyika katika sekta ya fedha pamoja na ushirikiano mkubwa kati ya serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo.

Maadhimisho hayo ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania yalikwenda sambamba na kongamano maalum lililowakutanisha magavana wa benki kuu kutoka nchi mbalimbali za Afrika, viongozi wa taasisi za fedha, wasomi na wadau wa maendeleo kujadili mageuzi ya kidijitali, sera za fedha na ustahimilivu wa uchumi katika mazingira ya mabadiliko ya dunia.