NA DENIS MLOWE NJOMBE

MRATIBU wa mbio za Uchumi Parachichi Marathon 2026, Respicius Mtabingwa, amesema maandalizi ya mbio hizo yanaendelea vizuri huku waandaaji wakijipanga kuhakikisha tukio hilo linakuwa jukwaa la kipekee la kutangaza zao la parachichi, kuhamasisha afya kwa wananchi na kufungua fursa za kiuchumi kwa wakulima wa Mkoa wa Njombe.

Akizungumza wakati wa ziara za uhamasishaji katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Njombe, Mtabingwa alisema kuwa mbio hizo zitafanyika Agosti 23, 2026 katika Viwanja vya Sabasaba mjini Njombe na zinatarajiwa kukutanisha washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Alisema tofauti na mashindano mengi ya riadha, Uchumi Parachichi Marathon imebeba dhamira pana zaidi ya kuunganisha michezo na maendeleo ya uchumi kupitia zao la parachichi ambalo limeendelea kuwa miongoni mwa mazao yanayochangia ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Njombe na taifa kwa ujumla.

“Mshindi atabeba tuzo kubwa, lakini lengo letu kuu ni kumtangaza mkulima bora na kuonyesha mchango wa zao la parachichi katika maendeleo ya wananchi. Tunataka dunia itambue kuwa parachichi si tunda tu, bali ni uchumi wa Njombe na chanzo muhimu cha lishe bora kwa jamii,” alisema Mtabingwa.

Alifafanua kuwa kaulimbiu ya mbio hizo ni “Parachichi ni Uchumi wa Njombe na Lishe Bora ya Mwanao”, ikiwa ni ujumbe unaolenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa zao hilo katika kuboresha kipato cha wakulima na afya za wananchi.

Mtabingwa alisema kuwa washiriki watapata nafasi ya kushiriki mbio katika umbali tofauti wa kilomita 42, 21, 10 na 5, hatua inayolenga kutoa nafasi kwa wanamichezo wa viwango mbalimbali pamoja na wananchi wa kawaida kushiriki katika tukio hilo.

Mbali na mashindano ya riadha, alisema kutakuwa na maonesho ya bidhaa za parachichi, elimu kuhusu kilimo bora, lishe, masoko ya ndani na nje ya nchi pamoja na fursa za uwekezaji zinazohusiana na zao hilo.

Alisema waandaaji wameandaa programu maalumu itakayowawezesha wakulima kukutana na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, wafanyabiashara, wasindikaji wa mazao na taasisi za kifedha ili kujadili namna ya kuongeza thamani ya zao la parachichi na kuboresha mnyororo wa thamani.

“Kwa kifupi tunasema huu siyo mkimbio wa kawaida. Hapa tunaleta vitu vitatu kwa pamoja; kukimbia, kujifunza na kucheza. Tunataka kila mshiriki aondoke akiwa amepata maarifa mapya, amefanya mazoezi na pia amefurahia burudani mbalimbali zitakazokuwepo siku hiyo,” alisema.

Mtabingwa aliongeza kuwa mbio hizo zinatarajiwa kuongeza mwamko wa utalii wa ndani kwa kuwa washiriki watapata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vya Mkoa wa Njombe huku wakijionea mashamba makubwa ya parachichi yanayolifanya eneo hilo kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa zao hilo nchini.

Alisema maandalizi yanafanyika kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali wa sekta za michezo, kilimo, biashara na utalii, huku lengo likiwa kuhakikisha tukio hilo linakuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Njombe.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi, taasisi, kampuni, wanamichezo na wadau wa maendeleo kujitokeza kwa wingi kushiriki na kudhamini tukio hilo ili kufanikisha azma ya kuitangaza Njombe na zao la parachichi katika viwango vya kitaifa na kimataifa.

“Njombe imebarikiwa kuwa na mazingira mazuri ya uzalishaji wa parachichi. Sasa ni wakati wa kutumia michezo kama daraja la kuitangaza fursa hii. Tunawakaribisha Watanzania wote kuja Njombe Agosti 23, 2026 kushiriki Uchumi Parachichi Marathon, kujifunza kuhusu parachichi na kushuhudia namna zao hili linavyoendelea kubadilisha maisha ya wakulima wetu,” alisema Mtabingwa.

Uchumi Parachichi Marathon 2026 inatarajiwa kuwa moja ya matukio makubwa ya michezo na uchumi katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, ikiwa na lengo la kuunganisha afya, kilimo, biashara na burudani katika jukwaa moja kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.