NA: MWANDISHI WETU, MWANZA 

Hakuna kulala. Hivi ndivyo unavyoweza kusema ndugu msomaji. Hii ni baada ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kuamua kukesha mitamboni hadi usiku wa manane kuhakikisha maji yanatoka kwa wakazi wa Jiji la Mwanza.Aweso amepiga kambi katika kituo cha kusukuma maji cha Capripoint usiku wa kuamkia Juni 15, 2026. 

Hii ni kufuatia agizo la Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba alilolitoa akiwa ziarani mkoani Singida. 

Dk. Mwigulu alimuagiza Aweso kufika Jijini Mwanza kuhakikisha maji yanatoka kwani amekuwa akipokea ujumbe kutoka kwa wananchi wakilalamikia ukosefu wa maji.

“Nimepokea meseji nyingi kuhusu tatizo la maji lililotokea Mwanza, nimemtuma Waziri aende haraka akasimamie jambo lile, ahakikishe mpaka maji yanapatikana,” amesema Dk. Mwigulu.

Katika hatua nyingine, Dk. Mwigulu ameonyesha kushangazwa na Jiji la Mwanza kukosa maji.

“Sisi watu wa Singida, Simiyu, Dodoma na Tabora tunataka kupata maji kutoka Mwanza, leo tunaambiwa Mwanza palepale kwenye Ziwa Victoria kuna shida ya maji, ni jambo ambalo haliwezi kueleweka na ni jambo ambalo sitaki kulisikia,” amesema.

Baada ya Aweso kufika Mwanza, ameongoza kikao kazi na Menejimenti ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA). 

Kikao hicho lilikuwa ni muhimu kabla ya kuanza ziara rasmi ya kukagua hali ya upatikanaji wa huduma ya maji Jijini humo. 

Aidha, Aweso anatarajia kutembelea chanzo cha maji Butimba kuona na kukagua upatikanaji wa maji. Ziara hiyo imemhusisha pia Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Mwajuma Waziri.