Na Mwandishi wetu,Mbinga

HALMASHAURI ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma imesema, itahakikisha inatenga fedha za kutosha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya michezo mashuleni ikiwemo viwanja ili kuwezesha wanafunzi kushiriki michezo mbalimbali na kuibua vipaji vyao.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Joseph Kashushura,wakati akipokea kikombe cha mshindi wa pili wa michezo kwa shule za sekondari Umiseta ngazi ya mkoa wa Ruvuma iliyomalizika jana ambapo Halmashauri ya wilaya Mbinga imeibuka mshindi wa pili wa ujumla huku nafasi ya kwanza ikishikwa na Manispaa ya Songea.

Aidha Kashushura,amewapongeza wanafunzi wa shule za sekondari walioshiriki mashindano hayo kwa kuiletea heshima kubwa Halmashauri ya wilaya Mbinga kwa kufanya vizuri na kufanikiwa kuwa mshindi wa pili na kuhaidi kuwaunga mkono katika mashindano yajayo ya Umeseta na Umitashumta ngazi ya mkoa na Taifa.

“Jambo hili limetupa faraja sana sisi viongozi tunaowasimamia vijana hawa,kama unavyofahamu michezo ni afya ukishiriki michezo hata kwenye masomo darasani unafanya vizuri,mimi kaka Mkurugenzi wa Halmashauri nawapongeza hawa vijana wetu”alisema Kashushura.

Alisema,ili kufanya vizuri zaidi kwenye mashindano yajayo tutaweka mikakati mizuri ikiwemo kuwawezesha walimu wa michezo kupata mafunzo maalum ili watakapokuja kuwafundisha vijana mashuleni waweze kufanya vizuri kwa kupata timu nyingi na imara ambazo zitaweza kushindana na timu za Halmashauri nyingine za mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.

Alisema,watasimamia mpango wa michezo mashuleni ili muda kuhakikisha wanafunzi wanapata muda wa kushiriki michezo mbalimbali ngazi ya shule ili kupata vijana wenye uwezo watakaoshiriki mashindano mbalimbali ndani na nje ya wilaya ya Mbinga kwa mafanikio makubwa.

Kashushura,amemuagiza afisa mipango wa Halmashauri hiyo khakikisha wanatenga bajeti ya kutosha ili kuboresha viwanja vya michezo ambavyo vitawezesha wanafunzi na vijana wengine kushiriki kwenye michezo na kuibua vipaji vyao.

Naye Afisa michezo wa Halmashauri hiyo Charles Maero alisema,Halmashauri ya wilaya Mbinga imeshika nafasi ya pili kimkoa baada ya kushiriki michezo mbalimbali ya Umiseta ngazi ya mkoa iliyofanyika katika Manispaa ya Songea kwa mwaka 2027.

Kiongozi wa timu za Halmashauri zlizoshiriki mashindano ya Umiseta ngazi ya mkoa mwalimu Francis Kyando alisema,wamekuwa washindi wa pili kati ya Halmashauri nane za mkoa wa Ruvuma kutokana na wanafunzi walioshiriki michezo mbalimbali kuonyesha vipaji na ari ya kupambana wakati wote.

Kyando alisema,kwa sasa kwenye shule nyingi ni ubovu wa miundombinu ya kuchezea hasa viwanja kwani kwenye shule nyingi viwanja vya kuchezea ni vibovu ambavyo haviruhusu vijana kuonyesha vipaji vyao.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake walioshiriki mashindano hayo Rose Haule,ameishukuru Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kwa kuwaandaa vizuri kushiriki michezo ya Umiseta mwaka huu na kuweza kuwa mshindi wa pili wa ujumla katika michezo yote na kuhaidi kufanya vizuri kwenye mashindano yajayo ya mwaka 2027.

Awali akifunga mashindano hayo wiki iliyopita katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Mary Makondo,aliwataka maafisa elimu,wakuu wa shule na waratibu elimu kuweka vipindi maalum vya michezo kila wiki mabvyo vitasaidia kuimarisha maandalizi na kuongeza ushindani wa michezo mashuleni.