*ACT WAZALENDO: Umoja ni Nguzo ya Mafanikio Yetu, Asema Prof. Omar Fakih Hamad
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya Chama cha ACT WAZALENDO, Profesa Omar Fakih Hamad, ambaye pia ni Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi kupitia chama hicho, amesema ACT WAZALENDO imeendelea kupata mafanikio katika chaguzi mbalimbali kutokana na mshikamano wa viongozi na wanachama wake.
Prof. Omar aliyasema hayo leo, Juni 14, 2026, huko Shangani, Mkokotoni, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kikatiba wa Jimbo la Kijini, Mkoa wa Kaskazini A, Unguja.
Alisema umoja uliopo ndani ya chama hicho umechangia kuimarika kwake kisiasa na kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za chama.
“Hali hii tunapaswa kuendelea kuiimarisha kwa maslahi ya chama na maendeleo ya wananchi wetu,” alisema Prof. Omar.
Akitolea mfano uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2015 katika Jimbo la Kijini, alisema wapiga kura walioandikishwa walikuwa 8,091 huku waliopiga kura wakiwa 6,095. Alisema mgombea wa CCM, Dkt. Mohammed Ali Shein, alipata kura 2,396 sawa na asilimia 41, wakati mgombea wa CUF aliyekuwa akiungwa mkono na ACT WAZALENDO, Maalim Seif Sharif Hamad, alipata kura 3,244 sawa na asilimia 56.
Aliwataka viongozi na wanachama wa Jimbo la Kijini kuendelea kudumisha mshikamano na kuepuka migawanyiko inayoweza kudhoofisha chama.
“Tukiendelea kuwa wamoja na kushirikiana, tutaendelea kuijenga na kuiimarisha ACT WAZALENDO,” alisema.
Aidha, aliwahimiza wananchi wa Jimbo la Kijini kushirikiana na wawakilishi wa ACT WAZALENDO katika kuwasilisha changamoto zinazowakabili ili zipatiwe ufumbuzi kupitia Baraza la Wawakilishi.
“Sisi kama wawakilishi tupo tayari kusikiliza na kufikisha changamoto za wananchi bila kujali tofauti za kisiasa,” alisema.
Kuhusu mazungumzo yanayoendelea kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT WAZALENDO, Prof. Omar alisema yanaendelea vizuri na kwamba viongozi wa vyama hivyo watatoa taarifa rasmi wakati utakapofika.
“Lengo ni kuendelea kuimarisha mshikamano na maslahi ya Wazanzibari,” alisema Prof. Omar.
Awali, Katibu wa Mipango na Uchaguzi wa Jimbo la Kijini, Hamad Abuu Hamad, alisema mkutano huo ulifikia akidi kwa kuhudhuriwa na wajumbe 122 kati ya wajumbe 191 waliotakiwa kuhudhuria kwa mujibu wa Katiba ya chama.
Alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya viongozi na wanachama wa jimbo hilo pamoja na Mkoa wa Kaskazini A.
Aidha, alisema licha ya changamoto mbalimbali, uongozi wa Jimbo la Kijini umeendelea kufanya ziara katika matawi yote kwa lengo la kuimarisha chama na kuendelea kuwafikia wananchi.

