Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema ziara ya Rais wa Singapore, Mheshimiwa Tharman Shanmugaratnam, nchini ni ya kihistoria kwa kuwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi huyo wa taifa hilo kuitembelea Tanzania tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili miaka 45 iliyopita.
Rais Samia amesema hayo leo Juni 9, 2026 katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya mazungumzo rasmi kati yake na Rais Shanmugaratnam yaliyojadili maeneo mbalimbali ya kimkakati kwa maendeleo ya mataifa hayo mawili.
Amesema ziara hiyo inaashiria dhamira ya pamoja ya Tanzania na Singapore ya kuimarisha zaidi ushirikiano wa kidiplomasia, biashara na uwekezaji kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo mbili.
“Tumejadili namna ya kuifanya mahusiano yetu yawe imara zaidi na yenye matokeo yanayoonekana kwa watu wetu. Ushirikiano wetu umeendelea kukua katika maeneo mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji, ufundi stadi, tamaduni na mipango miji,” amesema Rais Samia.
Aidha, amesema Tanzania imeiomba Singapore kufungua ubalozi wake nchini ili kuongeza kasi ya ushirikiano wa kidiplomasia na kurahisisha mawasiliano ya moja kwa moja kati ya mataifa hayo mawili.
Katika sekta ya biashara na uwekezaji, Rais Samia amesema kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Singapore bado hakijaendana na kiwango cha urafiki uliopo kati ya nchi hizo mbili, huku akibainisha kuwa thamani ya biashara iliyopo sasa ni dola za Marekani milioni 299 na uwekezaji kutoka Singapore ukiwa na miradi 36 nchini.
“Urafiki wetu ni mkubwa kuliko kiwango cha biashara tulichonacho sasa. Tumekubaliana kuongeza ushirikiano wa biashara na uwekezaji kuanzia sasa,” amesema.
Amesema pia nchi hizo mbili zimesaini mikataba mbalimbali ambayo itakuwa msingi wa kuimarisha ushirikiano katika sekta za uchumi, biashara na maendeleo ya wananchi.
Katika eneo la maendeleo ya vijana, Rais Samia amesema Tanzania imeiweka ajenda ya uwezeshaji wa vijana kuwa moja ya vipaumbele vikuu katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa kuwa vijana ndiyo watakaobeba uchumi na maendeleo ya taifa katika miaka ijayo.
Amesema serikali inalenga kuwawezesha vijana kupitia elimu, ukuzaji wa ujuzi, ujasiriamali, ubunifu pamoja na ushiriki mkubwa katika uchumi wa kidijitali ambao Tanzania imepanga kuuendeleza kwa kasi katika kipindi cha miaka kumi ijayo.
Kwa upande wa kilimo na usalama wa chakula, Rais Samia amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na Singapore katika uzalishaji wa mazao ya chakula kupitia mfumo wa uwekezaji wa kilimo cha uzalishaji kwa ajili ya masoko ya nje.
Amesema tayari Tanzania imeanza ushirikiano wa aina hiyo na Urusi katika uzalishaji wa ndizi na mazao mengine, huku akiikaribisha Singapore kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo nchini.
Rais Samia pia amepongeza nia ya Singapore kuanza mazungumzo ya ushirikiano wa biashara huria na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), akisema hatua hiyo itafungua fursa mpya za biashara na uwekezaji katika ukanda huo.
Kwa upande wake, Rais wa Singapore, Mheshimiwa Tharman Shanmugaratnam, amesema Tanzania ni lango muhimu la biashara na uwekezaji katika Afrika Mashariki kutokana na nafasi yake ya kimkakati, maendeleo ya Bandari ya Dar es Salaam pamoja na utulivu wake wa kisiasa.
Amesema Singapore inaiona Tanzania kama mshirika muhimu katika Afrika kutokana na ukuaji wa uchumi wake, idadi kubwa ya vijana na nafasi yake katika biashara ya kimataifa kupitia Bahari ya Hindi.
“Tanzania imeacha taswira kubwa kwangu. Ni taifa lenye kujiamini kuhusu uwezo wake na lenye nafasi muhimu katika mustakabali wa uchumi wa Afrika Mashariki,” amesema Rais Shanmugaratnam.
Aidha, amesema nchi yake ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika sekta za bandari, usafirishaji, uchumi wa kidijitali, usalama wa chakula pamoja na maendeleo ya ujuzi kwa vijana.
Ziara ya Rais wa Singapore nchini Tanzania inaendelea kuonekana kama hatua mpya ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya Afrika Mashariki na Asia ya Kusini-Mashariki huku Tanzania ikiendelea kujijenga kama kitovu muhimu cha biashara na uwekezaji katika ukanda huo.

