Mkurugenzi mwanzilishi wa kampuni ya Conserve Safari Camps & Lodges, Simon Mossi, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa sekta ya utalii na mchango wake katika kukuza uchumi wa Taifa.Mkurugenzi mwenza wa kampuni hiyo ,Einars Garoza akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha .

Happy Lazaro Arusha .

Arusha .UKUAJI unaoendelea kushuhudiwa katika sekta ya utalii nchini umeelezwa kuwa matokeo ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambazo zimechangia kuongeza hamasa ya uwekezaji, kutangaza vivutio vya utalii na kuvutia idadi kubwa ya watalii kutoka ndani na nje ya nchi.

Pongezi hizo zimetolewa jijini Arusha na Mkurugenzi mwanzilishi wa kampuni ya Conserve Safari Camps & Lodges, Simon Mossi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa sekta ya utalii na mchango wake katika kukuza uchumi wa taifa.

Mossi amesema kuwa katika miaka ya hivi karibuni sekta ya utalii imeendelea kukua kwa kasi na kuonyesha mafanikio makubwa, hali iliyowezesha wadau wengi wa sekta hiyo kunufaika kupitia ongezeko la wageni wanaotembelea maeneo mbalimbali ya utalii nchini.

Ameeleza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuitangaza Tanzania kimataifa, hususan kupitia filamu ya utalii ya The Royal Tour ambayo imeongeza uelewa wa dunia kuhusu vivutio vya kipekee vilivyopo nchini na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa maeneo yanayovutia watalii wengi zaidi.

Kwa mujibu wa Mossi, mazingira bora ya uwekezaji na ushirikiano uliopo kati ya Serikali na sekta binafsi yameendelea kuwapa wadau wa utalii fursa ya kuboresha huduma zao na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi na ajira.

Amesema kampuni ya Conserve Safari Camps & Lodges imeendelea kutoa huduma za malazi, ukarimu na chakula kwa viwango vya hali ya juu katika maeneo mbalimbali ya hifadhi, huku ikilenga kuhakikisha wageni wanaopokea huduma wanapata uzoefu bora wa utalii unaoendana na hadhi ya vivutio vya Tanzania.

Aidha, Mossi ametoa wito kwa Watanzania kuendeleza utamaduni wa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini, akisisitiza kuwa utalii wa ndani una nafasi kubwa katika kukuza sekta hiyo na uchumi wa taifa. Amesema ni muhimu wananchi wakajenga tabia ya kutembelea hifadhi za taifa, maeneo ya kihistoria na vivutio vingine vya asili ili kujionea urithi mkubwa ambao Tanzania imebarikiwa kuwa nao.

Kwa upande wake Mkurugenzi mwenza wa kampuni hiyo ,Einars Garoza amesema Tanzania inaendelea kuwa moja ya maeneo yanayokua kwa kasi katika sekta ya utalii kutokana na ongezeko kubwa la mahitaji kutoka soko la kimataifa.

 Amesema hali hiyo imefungua fursa nyingi za uwekezaji katika malazi, magari ya utalii na huduma za waongoza watalii.

Akizungumza na waandishi wa habari Garoza amesema kampuni yake imejikita katika kuendeleza uwekezaji wa malazi ya kitalii katika maeneo ya Serengeti na Tarangire, huku ikitarajia kupanua shughuli zake katika eneo la Ngorongoro.

 Amesema lengo lao ni kujenga maeneo yanayowawezesha wageni kuunganishwa na mazingira ya asili pamoja na kujitambua zaidi.

“Tanzania kwa sasa inashuhudia ongezeko kubwa la watalii linalozidi uwezo wa huduma zilizopo, jambo linalochochea wawekezaji kuingia katika sekta hiyo. “amesema .

Amebaainisha kuwa mahitaji ya malazi bora, magari ya safari na waongoza watalii wenye ujuzi yanaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Aidha, Garoza amesema kuwa, kampuni yake imekuwa ikitambulika kama miongoni mwa kéampuni zinazotoa huduma bora kwa gharama nafuu nchini Tanzania. 

Amefafanua kuwa falsafa yao ni kuhakikisha waendeshaji wa safari na kampuni za usimamizi wa watalii wanapata huduma za kiwango cha juu kwa bei inayomudu ushindani wa soko.

Amesema ana matumaini makubwa kuhusu mustakabali wa sekta ya utalii nchini, akibainisha kuwa ukuaji unaoendelea kushuhudiwa unaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa maeneo yenye mvuto mkubwa wa uwekezaji na utalii duniani.