Serikali imeendelea kusisitiza ushirikishwaji wa wananchi na wamiliki wa ardhi katika utekelezaji wa Mpango wa Uendelezaji Upya wa Eneo la Sinza jijini Dar es Salaam, unaotarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka 20 kuanzia mwaka 2026 hadi 2046.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wananchi wa Sinza ambao ni wadau wakuu wa mpango huo wanaendelea kushirikishwa katika hatua zote za utekelezaji kupitia mikutano ya uhamasishaji inayofanyika kuanzia ngazi za mitaa hadi ngazi za juu za maamuzi.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Bw. Eleuteri Mangi, imeeleza kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, ameendelea kuwataka wananchi wa Sinza kuwa makini na taarifa za upotoshaji zinazotolewa na watu wasiokuwa na nia njema kuhusu utekelezaji wa mpango huo.
Serikali imeeleza kuwa, uamuzi wa kuandaa mpango huo umetokana na ongezeko kubwa la watu mijini, ukuaji wa shughuli za kiuchumi pamoja na mahitaji ya maendeleo ya kisasa ya miji. Kupitia mpango huo, Sinza inatarajiwa kuwa kitovu cha makazi ya kisasa, biashara, huduma za kijamii na uwekezaji.
Wizara imebainisha kuwa, dhana ya uendelezaji upya wa maeneo ya miji si jambo jipya nchini na kuweka wazi kuwa, katika Jiji la Dar es Salaam, maeneo mbalimbali ikiwemo Posta, Upanga, Kariakoo, Magomeni, Oysterbay, Masaki, Ilala, Buguruni, Kurasini na Temeke yamewahi kupitia mabadiliko makubwa ya matumizi ya ardhi na shughuli za kiuchumi kutokana na mipango ya uendelezaji upya.
Maeneo hayo yamebadilika kutoka makazi yenye msongamano mdogo na kuwa vituo vya matumizi mchanganyiko vinavyojumuisha makazi, biashara, huduma mbalimbali na shughuli za kiuchumi. Pia yamepata majengo ya kisasa ya ghorofa nyingi, miundombinu bora na kuongezeka kwa thamani ya kiuchumi.
Serikali inaamini kuwa, utekelezaji wa Mpango wa Uendelezaji Upya wa Sinza utaongeza thamani ya eneo hilo, kuboresha mazingira ya kuishi kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa jiji na taifa kwa ujumla.
Aidha, mpango huo unaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa, teknolojia, ushindani wa miji na mazingira bora ya kuishi, huku ukichangia usalama, utulivu na ustawi wa wananchi.
