Na Happy Lazaro, Arusha
Mkoa wa Arusha unatarajiwa kuwa mwenyeji wa Michezo ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwaka 2026, baada ya maspika wa mabunge ya nchi wanachama kukubaliana kuwa mashindano hayo yafanyike jijini humo mwezi Desemba mwaka huu.
Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha dharura cha maspika wa mabunge ya EAC kilichoongozwa na Mwenyekiti wa kikao hicho, Amason Jeffah Kingi, ambaye ni Spika wa Bunge la Seneti ya Kenya
amesema mkutano huo uliitishwa mahsusi kujadili na kuamua nchi mwenyeji wa michezo hiyo ya kila mwaka inayowakutanisha wabunge kutoka nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Kingi amesema awali mashindano hayo yalipangwa kufanyika nchini Somalia, lakini yalikwama kutokana na changamoto za kiutawala na kiusalama.
Juhudi za kuyahamishia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo nazo hazikufanikiwa kutokana na changamoto za kiafya na milipuko ya magonjwa katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.
Ameeleza kuwa baada ya nchi mbalimbali kushindwa kuandaa mashindano hayo, maspika walifanya mashauriano na kufikia makubaliano ya pamoja ya kuipa Arusha jukumu la kuwa mwenyeji wa michezo hiyo, huku wakiahidi kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhakikisha maandalizi yanafanyika kwa ufanisi.
“Tumekubaliana kwamba michezo ya mwaka huu itafanyika Arusha mwezi Desemba. “amesema
Hii ni hatua muhimu katika kuimarisha mshikamano na ushirikiano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,” amesema Kingi baada ya kikao hicho.
Kwa upande wake, Daniel Sillo amesema Tanzania iliomba kutokuwa mwenyeji wa michezo hiyo kwa mwaka huu kutokana na majukumu makubwa ya kitaifa na kimataifa, ikiwemo maandalizi ya mkutano wa Inter-Parliamentary Union pamoja na maadhimisho ya miaka 100 ya Bunge la Tanzania.
Sillo amesema shughuli hizo zinahitaji maandalizi makubwa, hivyo Tanzania iliona ni busara kutoa nafasi kwa nchi nyingine kuandaa mashindano hayo, huku ikiendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za jumuiya hiyo.
Maspika hao pia wamekubaliana kukutana tena mwezi Agosti jijini Arusha kwa ajili ya kupitia hatua za maandalizi ya michezo hiyo pamoja na kujadili masuala mengine ambayo hayakupata nafasi ya kujadiliwa katika kikao cha dharura kilichofanyika sasa.

