Tuzo aliyokabidhiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kama kinara wa mabadiliko ya mifumo ya malipo nchini, si tu ishara ya heshima kwa Mkuu wa Nchi, bali ni tafsiri ya mafanikio ya sera, maono na msukumo wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuijenga Tanzania ya kidijitali.

Katika maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yaliyofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC) jijini Dar es Salaam, Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba, alieleza kuwa tuzo hiyo imetokana na mchango mkubwa wa Rais Samia katika kusukuma mbele mageuzi ya mifumo ya malipo, ujumuishaji wa huduma za kifedha pamoja na matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma.

Kauli hiyo ya BoT ina uzito mkubwa kwa kuwa taasisi hiyo ndiyo msimamizi mkuu wa sera za fedha, mifumo ya malipo na uthabiti wa sekta ya fedha nchini. Hivyo, kumpa Rais Samia tuzo hiyo kunamaanisha kuwa Benki Kuu imefanya tathmini ya kina na kubaini wazi kuwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, Tanzania imepiga hatua kubwa kuelekea uchumi wa kidijitali.

Kwa miaka mingi, mifumo ya malipo nchini ilikuwa ikikabiliwa na changamoto za urasimu, utegemezi mkubwa wa fedha taslimu na ukosefu wa muunganiko wa huduma kati ya taasisi mbalimbali. Hata hivyo, chini ya uongozi wa Rais Samia, Tanzania imeanza kushuhudia kasi mpya ya matumizi ya mifumo ya kidijitali katika sekta za umma na binafsi.

Moja ya maeneo yaliyopewa msukumo mkubwa ni matumizi ya mifumo ya malipo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ya serikali, malipo ya huduma, biashara za mtandaoni pamoja na huduma za benki na simu. Hatua hiyo imeongeza uwazi, kupunguza upotevu wa mapato na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Uchambuzi wa tuzo hiyo hauwezi kutenganishwa na msisitizo wa mara kwa mara wa Rais Samia kuhusu taasisi za serikali “kusomana” kidijitali. Katika mikutano na hotuba zake mbalimbali, Rais Samia amekuwa akisisitiza kuwa taasisi za serikali zinapaswa kuunganisha mifumo yao ili taarifa ziweze kupatikana kwa urahisi, huduma zitolewe kwa haraka na wananchi waondokane na adha ya kuzunguka kutoka ofisi moja hadi nyingine wakitafuta huduma.

Huu ulikuwa ujumbe muhimu wa kimkakati. Kwa tafsiri ya kiuchumi, “mifumo kusomana” kunamaanisha kujenga mazingira salama ya taasisi kushirikishana data na taarifa, jambo linalorahisisha biashara, ukusanyaji wa kodi, huduma za kifedha, usajili wa kampuni, utoaji wa leseni, bima, afya na hata huduma za kijamii.

Katika miaka ya karibuni, taasisi nyingi zimeanza kutekeleza kwa vitendo maelekezo hayo ya Rais Samia. Leo hii, mifumo mingi ya serikali imeunganishwa kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali. Wananchi wanaweza kufanya malipo kwa njia za kidijitali, kupata huduma mtandaoni na kutumia mifumo mbalimbali inayopunguza matumizi ya karatasi pamoja na urasimu.

Mageuzi hayo yamekuwa msingi muhimu wa ukuaji wa uchumi wa kidijitali, ambao sasa ni sehemu ya ushindani wa mataifa duniani. Uchumi wa kisasa unategemea kasi ya taarifa, usalama wa miamala na uwezo wa wananchi kufanya malipo kwa urahisi popote walipo. Ndiyo maana sekta ya fedha imeendelea kuwa mhimili muhimu wa mageuzi hayo.

Ni katika muktadha huo ambapo BoT imeona umuhimu wa kumtambua Rais Samia kama kinara wa mabadiliko ya mifumo ya malipo. Kwa mtazamo mpana, tuzo hiyo ni ishara kwamba Tanzania imeanza kujijengea mazingira bora ya kifedha yanayowezesha biashara, uwekezaji na ujumuishaji wa wananchi wengi zaidi katika mfumo rasmi wa uchumi.

Aidha, uwepo wa viongozi mbalimbali wa sekta ya fedha, mabalozi, wawakilishi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), magavana wa benki kuu kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), magavana wastaafu pamoja na taasisi za fedha za kimataifa katika maadhimisho hayo, unaonyesha kuwa hatua zinazochukuliwa na Tanzania zinaendelea kutambuliwa kimataifa.

Kwa upande mwingine, mageuzi haya yana mchango mkubwa katika kuijengea Tanzania taswira ya taifa linalokwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia duniani. Mfumo imara wa malipo si suala la benki pekee; ni msingi wa uchumi wa kisasa, biashara za mtandaoni, uwekezaji, ukusanyaji wa kodi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Hivyo basi, tuzo ya Rais Samia haiwezi kutazamwa kama hafla ya kawaida ya pongezi. Ni ujumbe unaoonyesha kuwa sera za Serikali ya Awamu ya Sita zimeanza kuzaa matokeo yanayoonekana katika sekta ya fedha na mifumo ya utoaji huduma. Aidha, ni uthibitisho kuwa maelekezo yake ya kuunganisha mifumo ya taasisi za serikali na kutumia teknolojia kwa ufanisi yameanza kubadili sura ya utoaji huduma nchini.

Kadiri Tanzania inavyoendelea kuelekea kwenye uchumi wa kidijitali, matarajio makubwa yataendelea kuwa katika kuimarisha usalama wa mifumo, kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya TEHAMA, kutoa elimu ya matumizi ya huduma za kidijitali kwa wananchi na kuhakikisha kuwa mageuzi hayo yanawanufaisha Watanzania wote mijini na vijijini.