Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma Bw. Omary Mhina, akizungumza wakati akifunga kikao kazi kukusanya maoni ya wadau kuhusu Rasimu ya Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi Endelevu, kilichoandaliwa na Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, katika ukumbi wa mikutano wa 8-8, mkoani Morogoro.
Afisa Ugavi Mwandamizi Wizara ya Fedha, Bw. Richard Benaya, akifafanua jambo kuhusu Rasimu ya Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi Endelevu wakati wa kikao kazi cha kukusanya maoni ya wadau kuhusu rasimu hiyo, kilichoandaliwa na Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, katika ukumbi wa mikutano wa 8-8, mkoani Morogoro.Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha Bw. Omary Mhina (mwenye shati jekundu), akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao kazi cha kukusanya maoni ya wadau kuhusu Rasimu ya Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi Endelevu, kilichoandaliwa na Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, katika ukumbi wa mikutano wa 8-8, mkoani Morogoro.
Na. Saidina Msangi, WF, Morogoro.
Wizara ya Fedha imewakutanisha wadau wa ununuzi na ugavi kutoka katika taasisi za umma nchini, katika kikao kazi cha uthibitisho wa Rasimu ya Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi Endelevu (2026 – 2037).
Pamoja na mambo mengine, kikao hicho kimelenga kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwa wadau hao, yanayolenga kuboresha na kuimarisha Mkakati huo kabla ya kuidhinishwa na kuanza kutekelezwa.
Akizungumza wakati akifunga kikao kazi hicho mkoani Morogoro, Kaimu Kamishna Msaidizi wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Bw. Omary Mhina, alisema lengo la kikao hicho ni kupata maoni ya wadau ili kuboresha rasimu ya mkakati ili kuimarisha usimamizi wa mnyororo wa ugavi, kuongeza uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma pamoja na kuzingatia misingi ya maendeleo endelevu.
‘‘Tumepokea maoni yote mliyoyatoa na sisi kama Wizara jukumu letu ni kwenda kuyafanyia kazi ili kuboresha maeneo yote tuliyoafikiana na kisha tutarejesha kwenu tena ili muweza kuhakiki kama yale yote tuliyokubaliana yamefanyiwa kazi’’, alisema Bw. Omari.
Aliongeza kuwa utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi Endelevu utasaidia taasisi nunuzi nchini kuendesha shughuli za mnyororo wa ugavi kwa ufanisi zaidi kwa kuzingatia malengo ya DIRA 2050, matakwa ya Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025 pamoja na Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410.
Wakizungumza kwa niaba ya washiriki wa kikao kazi hicho, Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi wa Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Morogoro na Rufiji, Bw. Arnold Mapinduzi, alisema kuwa ushiriki wa taasisi mbalimbali katika kupitia rasimu hiyo ni muhimu katika kuhakikisha masuala ya uhifadhi wa mazingira yanajumuishwa kikamilifu katika mifumo ya ununuzi na ugavi nchini.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi kutoka Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Bi. Upeo Sanga, amesema kikao hicho kimewapa wadau fursa ya kujadili na kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha rasimu ya Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi Endelevu wa mwaka 2026–2037 kabla ya kuidhinishwa na kuanza kutekelezwa.
Kikao hicho kilichowakutanisha washiriki kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Rufani za Zabuni za Umma, Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi, Chuo Kikuu Mzumbe, pamoja na wadau wengine muhimu katika mnyororo wa ugavi, kilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Dar to Moro, mkoani Morogoro kwa siku mbili kuanzia tarehe 11 hadi 12 Juni, 2026.
