Na John Bukuku – Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, ameeleza umuhimu wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchini Urusi, akisema kuwa ni sehemu muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza na waandishi wa habari Juni 7, 2026 jijini Dar es Salaam, Prof. Kitila amesema utekelezaji wa Dira ya 2050 unahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi. Amebainisha kuwa Tanzania itaendelea kutafuta wadau kutoka sehemu mbalimbali duniani ili kuhakikisha mafanikio ya dira hiyo. Aidha, ameongeza kuwa katika utekelezaji wa Dira hiyo, nchi haitachagua marafiki bali itashirikiana na mataifa mbalimbali kwa kuzingatia maslahi ya taifa.
Aidha, amebainisha kuwa katika ziara hiyo, Tanzania na Urusi zimekubaliana kushirikiana katika maeneo tisa ambayo ni kilimo, elimu na mafunzo, nishati, madini, viwanda, usafiri na usafirishaji, utalii, uchumi wa kidijitali pamoja na biashara na uwekezaji.
Pia amesema kuwa ushirikiano huo tayari umeanza kuzaa matunda kupitia kutiwa saini kwa hati nane za makubaliano, ikiwemo makubaliano kati ya Chuo Kikuu cha Mzumbe na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ya kuendeleza lugha za Kiswahili na Kirusi katika nchi hizo mbili. Aidha, amebainisha kuwa lugha ya Kirusi itaanza kufundishwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Vilevile, ameeleza kuwa Tanzania na Urusi zimesaini makubaliano kati ya Wizara ya Elimu ya Tanzania na Wizara ya Elimu ya Juu ya Shirikisho la Urusi kuhusu ushirikiano katika masuala ya elimu ya juu, sayansi, teknolojia na ubunifu.
Pia ameongeza kuwa kupitia Kituo cha Uwekezaji Maalum Tanzania (TISEZA), Tanzania imefanikiwa kuvutia uwekezaji katika maeneo ya madini, utalii, kilimo, uzalishaji wa dawa, miundombinu, mbolea na sekta ya fedha. Amebainisha kuwa mazungumzo yanaendelea na yanaelekea kukamilishwa kwa makubaliano katika maeneo sita, yakiwemo madini na makaa ya mawe, uanzishwaji wa kiwanda cha mbolea, kilimo cha ngano, ufugaji wa kuku, uchakataji na usafirishaji wa kahawa, miundombinu pamoja na uanzishwaji wa hoteli ya kitalii Ngorongoro.

