Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira ilipofanya ziara mapema mwaka huu kukagua ujenzi na ukarabati wa mfereji wa skimu ya umwagiliaji Lpwasi Ndorobo katika Halmashauri ya Iringa, ilishauri eneo hilo kuwepo na mradi wa biashara ya kaboni. Hii inaonyesha elimu ya biashara ya kaboni inavyoendelea kuwafikia wananchi wengi, hususan ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Picha kwa hisani ya Tovuti ya NCMC).
…………..
Na Hafidh Kido
MABADILIKO ya Tabianchi si dhana ngeni katika masikio ya Watanzania kwa sasa, hii ni kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakuwa salama kimazingira.
Machi 11, 2025 katika Mkutano Mkuu wa 39 wa Viongozi wa (ALAT – Association of Local Authorities of Tanzania) jijini Dodoma, Rais Dk. Samia aliwaeleza viongozi hao dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuboresha usimamizi wa biashara ya kaboni ili wananchi na halmashauri zenye rasilimali za misitu zipate manufaa.
Dhamira hii inatakiwa kuwafikia wananchi kuanzia viongozi wa juu ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata na Mitaa kwa lengo la kuamsha ari ya wananchi hasa waliopo vijijini kukimbia fursa ya biashara ya kaboni.
Biashara ya kaboni ni nini
Hewa ya kaboni dioksidi (CO₂) ni gesi inayopatikana kwa asili katika angahewa ya dunia.
Tangu Mapinduzi ya Viwanda kuanza mwishoni mwa karne ya 18, shughuli za binadamu kama uchomaji wa mafuta ya kisukuku (makaa ya mawe, mafuta na gesi asilia), ukataji wa misitu na baadhi ya shughuli za viwandani zimeongeza kiwango cha CO₂ angani kwa kiasi kikubwa.
Kwa mujibu wa ripoti ya Jopo la Kimataifa la Wanasayansi wa Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC – Intergovernmental Panel on Climate Change (2023). AR6 Synthesis Report: Climate Change 2023), shughuli za binadamu, hasa uzalishaji wa CO₂, ndizo sababu kuu za ongezeko la joto duniani.
Kwa kawaida, nishati kutoka jua hupenya katika angahewa na kufika kwenye uso wa dunia. Dunia inapopata joto, hutoa sehemu ya nishati hiyo kama mionzi ya joto (infrared radiation) kuelekea angani. Gesi za chafu kama CO₂ hufyonza sehemu ya mionzi hii na kuirejesha tena kuelekea uso wa dunia. Matokeo yake ni kuongezeka kwa joto katika mfumo wa dunia, hali inayojulikana kama greenhouse effect.
IPCC inafafanua kuwa shughuli za binadamu zimeongeza kiwango cha CO₂ kutoka takribani sehemu 280 kwa milioni (ppm) kabla ya Mapinduzi ya Viwanda hadi zaidi ya ppm 420 katika miaka ya karibuni.
Biashara ya kaboni ilizaliwa ndani ya mfumo wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) ulioanzishwa mwaka 1992. Lengo kuu la mkataba huo lilikuwa kudhibiti ongezeko la gesi chafuzi angani ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hatua muhimu katika maendeleo ya biashara ya kaboni ilifikiwa mwaka 1997 kupitia makubaliano ya mkutano uliofanyika Japan, maarufu Kyoto Protocol.
Chini ya itifaki hii, nchi zilizoendelea zilipewa malengo ya lazima ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafu. Ili kurahisisha utekelezaji wa malengo hayo kwa gharama nafuu, Kyoto Protocol ilianzisha mifumo mitatu ya soko: Emissions Trading, Joint Implementation (JI), na Clean Development Mechanism (CDM).
Mwaka 2015, dunia ilipitisha makubaliano ya Paris au Paris Agreement, ambayo ilileta mfumo mpya wa ushirikiano wa kimataifa katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Chini ya Kifungu cha 6 (Article 6) cha Paris Agreement, nchi ziliruhusiwa kushirikiana katika biashara ya kaboni kupitia mifumo mipya ya uhamishaji wa matokeo ya upunguzaji wa hewa ukaa na soko jipya la mikopo ya kaboni linalosimamiwa chini ya UNFCCC.
Mwaka 2021 katika mkutano wa COP26 uliofanyika Glasgow, nchi wanachama wa UNFCCC zilikubaliana kanuni muhimu za utekelezaji wa Article 6, hatua iliyofungua njia ya kuanzishwa kwa soko jipya la kaboni chini ya Paris Agreement. Mfumo huu unalenga kuhakikisha uwazi, uadilifu wa mazingira na kuzuia kuhesabu punguzo la uzalishaji mara mbili.
Tanzania imepokea mkakati huu
Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis, aliliambia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2025 kuwa Tanzania ilikuwa tayari imepata takribani Shilingi bilioni 45 kutokana na biashara ya kaboni. Fedha hizo zilikuwa zimeanza kunufaisha wananchi katika halmashauri 10 nchini.
Kufikia Januari 2026 idadi hiyo iliongezeka na kufikia miradi 82 iliyosajiliwa, ambapo miradi minne ilikuwa imeingia katika hatua ya utekelezaji kamili.
Aidha, moja ya mafanikio makubwa ya biashara ya kaboni nchini Tanzania ni Mradi wa Ntakata Mountains uliopo Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi. Mwaka 2024 pekee, vijiji vinavyoshiriki mradi huo vilipata Shilingi bilioni 14.25.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (National Carbon Monitoring Centre – NCMC), Catherine Kigaraba, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zilizoanzisha kanuni maalumu za biashara ya kaboni kupitia Kanuni za Udhibiti na Usimamizi wa Biashara ya Kaboni za mwaka 2022 pamoja na marekebisho ya mwaka 2023. Miradi yote lazima isajiliwe na ihusishe jamii za wenyeji katika utekelezaji wake.
Miradi iliyosajiliwa imegawanyika katika sekta mbalimbali: Misitu asilimia 51, Nishati asilimia 33, Kilimo asilimia 8, Mifugo asilimia 5 na Usimamizi wa taka asilimia 3.
Mwandishi wa makala haya katika mahojiano maalum na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, Onesmo Buswelu, amejifunza kuwa biashara ya kaboni katika Wilaya ya Tanganyika ilianza rasmi mwaka 2018 kwa vijiji vinane ambavyo ni Lwega, Lugonesi, Mpembe, Bujombe, Kapanga, Kagunga, Katuma na Mwese.
Vijiji hivyo viliingia mkataba na Kampuni ya Carbon Tanzania wa unyonyaji wa kaboni na kuuzwa kwenye soko la hiari kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa ya kudhibiti mabadiliko ya tabianchi kwa kupunguza ongezeko la joto duniani.
“Biashara hii inahusisha misitu ya vijiji hivi vinane yenye ukubwa wa hekta 216,944 za ardhi na wakazi zaidi ya 34,242 wanaofaidika na biashara hiyo. Halmashauri pamoja na vijiji hivi vimeshanufaika kwa mapato ya biashara ya kaboni ambapo katika kipindi cha awamu ya kwanza hadi ya kumi na mbili jumla ya Shilingi 30,936,371,130.45,” anaeleza Buswelu.
Mkuu huyo wa wilaya anafafanua kuwa maeneo yaliyonufaika kupitia fedha hizo ni pamoja na sekta ya afya, elimu, kilimo, viwanda na biashara.
SEKTA YA AFYA
Ujenzi wa Kituo cha Afya Katuma kwa kujenga majengo ya mama na mtoto, maabara, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la kufulia na jengo la wagonjwa wa nje (OPD).
Ununuzi wa vifaa tiba na dawa kwa zahanati za vijiji vya Katuma, Kapanga, Lwega, Mpembe, Kagunga, Lugonesi na Bujombe vyenye thamani ya Shilingi 700,000,000.
Ujenzi wa zahanati ya Kitongoji cha Manyonyi.
SEKTA YA KILIMO
Ujenzi wa majosho matatu kwa vijiji vya Kapanga, Lwega na Bujombe.
SEKTA YA ELIMU MSINGI
Ujenzi wa vyumba 55 vya madarasa katika vijiji vinane vya mradi wa kaboni.
Ukarabati wa vyumba 19 vya madarasa katika vijiji hivyo.
Ujenzi wa nyumba tisa za walimu (two in one) na nyumba mbili za walimu (single).
Ujenzi wa matundu 120 ya vyoo katika shule za msingi pamoja na utengenezaji wa madawati 1,496.
SEKTA YA ELIMU SEKONDARI
Ujenzi wa Sekondari ya Bujombe.
Ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na vyoo vya matundu manane katika Sekondari ya Bujombe.
Ujenzi wa bwalo la chakula pamoja na jiko katika Sekondari ya Mwese.
Ujenzi wa mabweni mawili ya wavulana na wasichana katika Sekondari ya Mwese.
SEKTA YA UTAWALA
Ujenzi wa nyumba nane za watendaji wa vijiji vya biashara ya kaboni.
Ujenzi wa ofisi nane za vijiji pamoja na ofisi moja ya Kata ya Kasekese.
Mafanikio mengine ni uwezeshwaji wa wananchi kiuchumi kupitia COCOBA kwa vikundi 47 vya kijamii katika vijiji vya biashara ya kaboni pamoja na ununuzi wa magari mawili ya kusimamia misitu.
SEKTA YA VIWANDA NA BIASHARA
Ujenzi wa masoko matatu katika vijiji vya Katuma, Mwese na Lugonesi.
Ujenzi wa vyumba 10 vya maduka katika Kijiji cha Katuma.
Haya yote yamefanyika katika Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi kwa fedha zilizopatikana katika biashara ya kaboni.
Nini kifanyike ili wilaya nyingine ziige mfano huu
Mwandishi wa makala haya katika mahojiano maalumu na Mkurugenzi wa NCMC, Catherine Kigaraba, alitaka kujua mbinu zinazotumika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu biashara ya kaboni.
“Ni ukweli ulio wazi kuwa biashara ya kaboni ni jambo jipya kwa Watanzania, hata hivyo serikali kupitia kituo chake cha kuratibu biashara ya kaboni inatumia mbinu mbalimbali kupeleka elimu kwa ngazi zote za jamii wakiwemo wananchi wa kawaida,” anaeleza Kigaraba.
“Kwanza ni elimu kupitia vyombo vya habari kama runinga, redio na magazeti. Pia mitandao ya kijamii kupitia kurasa rasmi za kituo ikiwemo Instagram na Facebook.”
Amebainisha kuwa tovuti rasmi ya kituo pia hutoa taarifa mahususi za biashara ya kaboni kila wakati bila kusahau majukwaa ya maonyesho rasmi ya kitaifa kama Wiki ya Mazingira Duniani, Wiki ya Utumishi wa Umma, Decarbonization Day pamoja na Sikukuu ya Wakulima (Nanenane).
“Upo mkakati maalumu wa kupeleka uelewa wa biashara ya kaboni kwa wadau wote wakiwemo wabunge, TAMISEMI, makatibu wakuu, wanafunzi wa vyuo na wadau wengine wa mazingira.”
Hata hivyo, inaonekana kuna fedha nyingi zimeshindwa kuingizwa katika mfumo wa biashara ya kaboni kutokana na ufuatiliaji duni.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyochapishwa mwaka 2025 ilieleza kuwa Tanzania ilikosa mapato yanayokadiriwa kufikia Shilingi trilioni 1.26 kutokana na uratibu hafifu, uelewa mdogo na kuchelewa kwa baadhi ya miradi ya biashara ya kaboni.
Hii inaonyesha kuwa sekta hiyo bado ina nafasi kubwa ya kukua zaidi.
