Dodoma.
Wizara ya Madini kupitia Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini imeshiriki kikamilifu katika zoezi la ufuatiliaji wa utekelezaji wa miongozo ya Ufuatiliaji na Tathmini, utendaji wa Wizara pamoja na utekelezaji wa maelekezo mbalimbali ya Serikali, zoezi lililoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Zoezi hilo lilifanyika katika Ofisi za Wizara ya Madini zilizopo Mtumba, Jijini Dodoma Juni 2, 2026, likiwa na lengo la kutathmini hali halisi ya utekelezaji wa shughuli za ufuatiliaji na tathmini, kupima ufanisi wa mifumo iliyowekwa, kubaini changamoto zinazoweza kuathiri utekelezaji wa majukumu ya Wizara pamoja na kutoa mapendekezo ya maboresho yatakayosaidia kuimarisha utendaji na uwajibikaji wa taasisi.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Menrad Seluhinga, alisema kuwa ufuatiliaji na tathmini ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha mifumo ya usimamizi wa utendaji wa Wizara inaendelea kuimarika na kuendana na matakwa ya Serikali katika kusimamia utekelezaji wa mipango na miradi ya maendeleo.
Alieleza kuwa kupitia zoezi hilo, Wizara zimepata fursa ya kujitathmini na kubaini maeneo yanayohitaji kuimarishwa ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa wakati, kwa ufanisi na kwa kuzingatia matumizi sahihi ya rasilimali za umma.
“Ufuatiliaji na tathmini ni sehemu muhimu katika mzunguko wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwani husaidia kupima mafanikio yaliyopatikana, kubaini changamoto zilizopo na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha utoaji wa huduma na utekelezaji wa majukumu ya Wizara,” alisema Seluhinga.
Katika zoezi hilo, uchambuzi wa maeneo mbalimbali muhimu yanayohusiana na usimamizi wa ufuatiliaji na tathmini pamoja na utendaji wa Wizara ulifanyika. Maeneo hayo ni pamoja na upatikanaji na matumizi ya nyaraka muhimu za na utekelezaji wa maelekezo ya Serikali na maeneo mengine.
Maeneo mengine yaliyofanyiwa tathmini ni utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Wizara, ufuatiliaji wa utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III), utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na usimamizi wa kero na malalamiko yanayohusu huduma na utendaji wa Wizara.

