Mkurugenzi wa hoteli za kitalii za Masai Safari Lodge Arusha na Masailand Coffee Lodge Karatu, Dkt. Charles Becon akizungumza na waandishi wa  habari kwenye maonesho hayo.
………….
Na Happy Lazaro, Arusha
Maonesho ya Kimataifa ya Karibu-KiliFair yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kutangaza huduma za utalii na ukarimu, huku wadau mbalimbali wa sekta hiyo wakitumia fursa hiyo kuonesha bidhaa na huduma wanazotoa kwa soko la ndani na la kimataifa.
Mkurugenzi wa hoteli za kitalii za Masai Safari Lodge Arusha na Masailand Coffee Lodge Karatu, Dkt. Charles Becon, amesema maonesho hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii Afrika Mashariki pamoja na kuwapa wafanyabiashara nafasi ya kukutana na wateja na washirika wapya wa biashara.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho hayo  yanayofanyika jijini Arusha, Dkt. Becon amewapongeza waandaaji wa maonesho hayo kwa kuendelea kuyaendesha kwa kiwango cha kimataifa na kuvutia washiriki kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Amesema ushiriki wao katika maonesho hayo unalenga kutangaza huduma zinazotolewa na Masai Safari Lodge Arusha, Masailand Coffee Lodge Karatu pamoja na Tanga Beach Resort, ambazo zimeendelea kuwahudumia watalii wa ndani na nje ya nchi kwa viwango vya hali ya juu.
“Karibu-KiliFair imekuwa sehemu muhimu ya kutangaza biashara za utalii. Tumekuja kuonesha huduma na bidhaa zetu, kukutana na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii na kujenga ushirikiano mpya utakaosaidia kukuza biashara na utalii kwa ujumla,” amesema Dkt. Becon.
Ameongeza kuwa maonesho hayo yamekusanya idadi kubwa ya washiriki kutoka maeneo mbalimbali duniani, jambo linaloonesha namna Tanzania inavyoendelea kujijengea nafasi katika soko la utalii la kimataifa. Alisema kupitia jukwaa hilo, wadau wa utalii wanapata nafasi ya kutangaza huduma zao moja kwa moja kwa wanunuzi wa huduma za utalii na wawekezaji.
Dkt. Becon amesema hoteli hizo zimeendelea kuboresha huduma zake ili kuwapatia wageni mazingira bora ya mapumziko na uzoefu wa kipekee wa kutembelea vivutio vya utalii vya Tanzania, huku akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya wadau wa sekta hiyo ni muhimu katika kuendeleza mchango wa utalii katika uchumi wa taifa.
Aidha, alieleza matumaini yake kuwa maonesho ya Karibu-KiliFair yataendelea kuwa kichocheo cha ukuaji wa biashara za utalii na ukarimu nchini kwa kuunganisha wadau wa ndani na wa kimataifa katika kutangaza fursa zilizopo Tanzania