WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amehitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Iringa kwa kuwataka viongozi na watumishi wa umma kuendelea kusimamia haki, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi pamoja na kufuatilia utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa katika kutatua kero za wananchi.
Ametoa maelekezo hayo leo Jumapili (Juni 7, 2026) wakati akifunga ziara yake ya kikazi mkoani Iringa kwa kufanya kikao cha majumuisho na viongozi pamoja na watumishi wa umma kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Dkt. Mwigulu amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi katika sekta mbalimbali za maendeleo hivyo ni wajibu wa viongozi na watumishi kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na haki zao zinalindwa.
Amesema ameridhishwa na namna Mkoa wa Iringa ulivyoshughulikia changamoto mbalimbali za wananchi na kuwataka viongozi kuendelea kuwa mbele ya matukio kwa kusikiliza na kutatua kero kabla hazijafikia hatua kubwa.
“Nimeona viongozi wa Mkoa wa Iringa wako mbele ya matukio. Kila hoja iliyojitokeza tayari ilikuwa imepokelewa na hatua mbalimbali zilikuwa zimeanza kuchukuliwa. Huo ndiyo mwelekeo ambao Serikali inautaka,” alisema.
Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa Mkoa huo kufuatilia moja baada ya nyingine kero zote zilizowasilishwa katika ziara yake na kuhakikisha wananchi wanapata mrejesho wa hatua zinazochukuliwa.
Alisema Serikali itaendelea kufanya tathmini ya utekelezaji wa maelekezo hayo na kwamba viongozi wa mikoa na halmashauri wanapaswa kuweka kumbukumbu za utekelezaji wa kila hoja iliyowasilishwa na wananchi.
Katika sekta ya afya, Dkt. Mwigulu alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha dawa muhimu na vifaa tiba vinapatikana kulingana na mahitaji ya maeneo husika pamoja na kuimarisha usimamizi wa fedha zinazotengwa kwa ajili ya huduma za afya.
Aidha, alizitaka halmashauri na taasisi za umma kuendelea kuwasaidia watu wenye ulemavu, wazee wasiojiweza na makundi mengine maalum kwa kutumia rasilimali zilizopo ili kuboresha ustawi wao.
Kwa upande wa miundombinu, Waziri Mkuu alielekeza kuharakishwa kwa utekelezaji wa miradi ya barabara iliyo katika hatua mbalimbali za maandalizi na utekelezaji huku akisisitiza ujenzi wa miundombinu yenye viwango vinavyoweza kuhimili changamoto za mazingira.
Pia aliwataka viongozi kuendelea kutatua migogoro ya ardhi kwa haki na kwa kuzingatia sheria pamoja na kuhimiza wananchi kurasimisha umiliki wa mali zao ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza baadaye.
Akizungumzia utendaji wa watumishi wa umma, Dkt. Mwigulu alisema ni muhimu kuwatambua na kuwathamini watumishi wanaofanya kazi kwa uadilifu na ufanisi huku hatua stahiki zikichukuliwa kwa wale wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao.
“Haki, uwajibikaji na huduma bora kwa wananchi lazima viwe msingi wa utendaji wetu. Wananchi wanatarajia kuona matokeo ya kazi zetu na ndiyo dhamira ya Serikali,” alisema.
Aidha, Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa mkoa huo kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo yote aliyoyatoa katika ziara hiyo ikiwemo migogoro ya ardhi, madai ya wananchi dhidi ya taasisi na kampuni mbalimbali, pamoja na masuala ya ustawi wa jamii yaliyowasilishwa katika mikutano ya hadhara.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James alisema ziara ya Waziri Mkuu imeimarisha ari ya uwajibikaji kwa viongozi na watumishi wa umma pamoja na kutoa mwelekeo wa kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo.

