Na Sophia Kingimali.
Chuo cha Ufundi cha Furaika Education College kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kimezindua mpango maalum wa kutoa mafunzo ya ufundi kwa vijana wenye mahitaji maalum, hatua hiyo inayolenga kuhakikisha kundi hilo linapata fursa sawa za elimu na ujuzi wa kujitegemea.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. David Msuya, alisema ushirikiano huo unaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kuongeza upatikanaji wa elimu jumuishi kwa Watanzania wote bila kujali hali zao za kimwili.
Alisema chuo hicho, ambacho ni miongoni mwa taasisi zinazotoa mafunzo ya ufundi bila malipo kwa wanafunzi, kimeweka mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu mbalimbali ikiwemo wenye matatizo ya kusikia, kutembea na changamoto nyingine za kimwili.
“Ulemavu si kigezo cha kumzuia mtu kupata elimu ya ufundi. Tumejipanga kuwa na walimu wa saikolojia, walimu wa lugha ya alama pamoja na mazingira yanayowezesha kila mwanafunzi kujifunza kwa urahisi,” alisema Dkt. Msuya.
Aliongeza kuwa chuo hicho kinapokea vijana wenye mahitaji maalum pamoja na wale wasiokuwa na changamoto za ulemavu, huku kikisisitiza kuwa mafunzo yote yanatolewa bila ada ili kuwapa nafasi vijana wanaoshindwa kuendelea na masomo kutokana na changamoto za kiuchumi.
Dkt. Msuya alizitaka taasisi, mashirika ya kiraia na wadau wanaohudumia watu wenye ulemavu kushirikiana na chuo hicho kwa kuwapeleka vijana wanaohitaji mafunzo ili waweze kujengewa uwezo wa kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Alisema changamoto kubwa inayowakabili vijana wengi wenye mahitaji maalum ni ukosefu wa msaada wa kugharamia mahitaji madogo ya kielimu, ikiwemo ada ya mitihani, jambo ambalo linawafanya baadhi yao kushindwa kujiunga na mafunzo licha ya kuwa na uwezo na hamu ya kusoma.
Aidha Dkt. Msuya amesema chuo hicho kinatoa mafunzo mbalimbali ya ufundi yakiwemo ususi, teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT), umeme, hoteli na utalii pamoja na ushonaji wa viatu, fani ambazo zina uwezo wa kuwawezesha wahitimu kujiajiri mara baada ya kumaliza masomo.
Alisema lengo la ushirikiano huo na Wizara ya Elimu ni kuhakikisha hakuna kijana mwenye mahitaji maalum anayebaki nyumbani kwa kukosa fursa ya elimu au ujuzi wa kazi.
Aidha, amewahimiza wazazi na walezi wenye watoto wenye changamoto mbalimbali kutumia fursa hiyo kwa kuwapeleka chuoni ili waweze kutimiza ndoto zao za kielimu na kiuchumi.
“Tunataka kuona vijana wote wanapata nafasi ya kujifunza na kujitegemea. Kupitia ushirikiano wetu na Wizara ya Elimu tunaamini tutafikia vijana wengi zaidi na kuwajengea uwezo wa kushiriki katika maendeleo ya jamii,” alisema.
Hatua hiyo inatajwa kuwa sehemu ya jitihada za kuimarisha elimu jumuishi nchini na kuongeza fursa za mafunzo ya ufundi kwa makundi maalum, sambamba na kukuza ajira na kujiajiri miongoni mwa vijana.
