Na Mwandishi wetu, Babati
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Civic Social Protection Foundation (CSP) na Vi Agroforestry wameadhimisha siku ya mazingira duniani kwa kupanda miti 1,200 na kufanya shughuli mbalimbali za uhifadhi wa mazingira Mjini Babati, Mkoani Manyara.
Mwanasheria wa CSP Eliakim Paul, akizungumza kwenye maadhimisho hayo ameeleza kuwa shirika hilo hiyo limeendelea kushirikiana na jamii katika juhudi za kulinda mazingira kupitia upandaji miti, elimu ya mazingira na shughuli za usafi.
Eliakim amesema katika maadhimisho ya mwaka huu wa 2026 wamepanda miti 1,200 ya matunda, mbao na kivuli kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo shule ya msingi Malangi, zahanati ya Malangi, shule za sekondari FT Sumaye na Himiti na ofisi ya kijiji cha Himiti.
Amesema pia wamegawa miti hiyo kwa mtu mmoja mmoja ili kuhamasisha utunzaji wa mazingira katika ngazi ya familia na jamii kwa ujumla.
“Sambamba na zoezi la upandaji miti, shughuli za usafi wa mazingira zimefanyika katika shule za sekondari za FT Sumaye na Himiti, katika kuunga mkono juhudi hizo, CSP ilitoa mapipa ya taka kwa ajili ya kuhifadhia taka na kusaidia kudumisha usafi wa mazingira shuleni,” amesema.
Amesema madhimisho hayo yalipambwa na mdahalo maalumu uliowashirikisha wanafunzi wa shule za sekondari za FT Sumaye na Himiti.
“Wanafunzi hao waliandika insha kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na usafi wake, ambapo mada hizo zilijadiliwa zaidi kupitia mdahalo ulioboreshwa kwa michango mbalimbali kutoka kwa wanafunzi wenzao pamoja na watu waliohudhuria hafla hiyo iliyofanyika katika shule ya sekondari Himiti,” amesema.
Mwakilishi wa ofisa mazingira wa mkoa wa Manyara, Aretas Laurent amewahamasisha watu kuendelea kupanda miti na kufanya usafi wa mazingira, mara kwa mara ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Laurent amehamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira kwa kupanda miti na kufanya usafi wa mazingira mara kwa mara.
Amerejea mafundisho kutoka katika Biblia na Qur’an akieleza kuwa Mwenyezi Mungu alipoumba mbingu na nchi aliumba mazingira mazuri, ila shughuli za binadamu zimekuwa zikibadilisha uhalisia wake.
Amesisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana kwa pamoja katika kuijenga Tanzania yenye mazingira ya kijani kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mwakilishi huyo wa mgeni rasmi ameeleza kuwa uongozi wa mkoa wa Manyara unatambua mchango mkubwa unaotolewa na CSP na Vi Agroforestry katika masuala ya uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Katika kuhitimisha shughuli hizo, zawadi mbalimbali zilitolewa kwa wanafunzi walioshiriki mdahalo huo pamoja na vyeti vya pongezi kutolewa kwa shule za sekondari za FT Sumaye na Himiti kwa ushiriki wao mzuri katika maadhimisho hayo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Himiti, Necodemasi Lohay Tsere ametoa shukrani za dhati kwa CSP na Vi Agroforestry kwa kuona umuhimu wa kushirikisha eneo lake katika shughuli za utunzaji wa mazingira.
Tsera ameeleza kuwa shule ya sekondari Himiti bado ni mpya, hivyo inahitaji miti mingi zaidi ili kuifanya kuwa na mazingira ya kijani na ya kuvutia kwa wanafunzi kujifunzia.
Katika tukio hilo walimu wakuu wa shule husika, msimamizi wa zahanati, wanafunzi na watu waliohudhuria walitoa shukrani zao na kuonesha hamasa kubwa ya kuendelea kutunza mazingira kupitia upandaji na utunzaji wa miti na kufanya usafi wa mazingira mara kwa mara.
