Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwasili katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete Mkoani Dodoma kushiriki Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, leo tarehe 05 Juni 2026.Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akitembelea na kukagua mabanda mbalimbali ya maonesho kuhusu shughuli za uhifadhi mazingira, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete mkoani Dodoma, leo tarehe 05 Juni 2026.Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akisikiliza maelezo kutoka kwa Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Manyinga ya Mvomero, Morogoro, Jackline Eliabi kuhusu utumiaji wa taka katika kutengeneza bidhaa mbadala, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete mkoani Dodoma, leo tarehe 05 Juni 2026.Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akisikiliza maelezo kutoka kwa Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Dumila Juu ya mkoani Morogoro, Alhad Yusuph kuhusu matumizi ya michezo katika kuhamasisha utunzaji mazingira, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete mkoani Dodoma, leo tarehe 05 Juni 2026.Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwa na viongozi mbalimbali wakiwa katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete wakishiriki Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani tarehe 05 Juni 2026.

…………..

Na John Bukuku, Dodoma

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itaendelea kuimarisha juhudi za uhifadhi wa mazingira nchini ili kuhakikisha Tanzania inakuwa salama dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira.

Dkt. Nchimbi ameyasema hayo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma, ambapo alisisitiza kuwa suala la mazingira ni ajenda muhimu ya maendeleo endelevu kwa taifa.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kulinda mazingira sambamba na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, akionya kuwa uharibifu wa mazingira una athari kubwa kwa afya za wananchi, uchumi pamoja na ustawi wa jamii.

“Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha tunalinda mazingira yetu kwa vitendo kwa sababu mazingira bora ni msingi wa maendeleo ya taifa letu,” amesema Dkt. Nchimbi.

Aidha, amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi wa mazingira ikiwemo upandaji miti, utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na matumizi ya nishati safi ili kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira.

Makamu wa Rais amesema maadhimisho ya mwaka huu yamekuwa sehemu muhimu ya kuhamasisha jamii kuchukua hatua dhidi ya changamoto za taka za plastiki na uharibifu wa mazingira unaochangiwa na shughuli za kibinadamu.

Pia ameahidi kuwa Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na kanuni za mazingira ili kuhakikisha rasilimali za asili zinalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhandisi Yusuf Masauni amesema Tanzania inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto za mazingira kupitia utekelezaji wa sera, mikakati na programu za uhifadhi wa mazingira nchini.

Mhandisi Masauni amesema maadhimisho hayo yamebeba ujumbe wa kuhamasisha wananchi na wadau mbalimbali kushiriki katika mapambano dhidi ya uchafuzi wa mazingira unaoongezeka duniani.

“Tunahitaji ushiriki wa kila mwananchi katika kuhakikisha mazingira yetu yanakuwa salama na endelevu kwa manufaa ya taifa letu,” amesema Mhandisi Masauni.

Ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi wa taka ngumu, uhifadhi wa misitu pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira katika sekta mbalimbali za uzalishaji na huduma.

Aidha, amesema Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kutoa elimu ya mazingira kwa wananchi ili kujenga uelewa mpana kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira na athari zinazoweza kujitokeza endapo juhudi za uhifadhi hazitapewa kipaumbele.

Katika maadhimisho hayo, viongozi wa serikali, taasisi mbalimbali pamoja na wadau wa mazingira walitembelea mabanda ya maonesho yaliyobeba ubunifu na teknolojia mbalimbali za utunzaji wa mazingira huku wakitoa wito kwa jamii kuendelea kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira nchini.