Waaswa kuwa Mabalozi wazuri na kuzingatia maadili

Naibu Karibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Zuhura Yunus, amewaasa vijana 756 wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania kwa kudumisha mshikamano na kuonyesha maadili bora.Amesema hayo Mei 22, 2026 jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwaaga vijana hao, amesema “Kila mmoja wenu anabeba taswira ya Taifa letu, hivyo ni wajibu wenu kuonyesha nidhamu, bidii na mshikamano ili kuendeleza heshima ya Tanzania.”

Ameongeza kuwa, tangu mwaka 2022 hadi Mei 21, 2026, jumla ya watanzania 14,057 wameunganishwa na fursa za ajira nje ya nchi. Aidha, Serikali inaendelea kukamilisha usaili wa nafasi 300 za wauguzi watakaokwenda kufanya kazi katika Serikali ya Saudi Arabia.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira, Bi. Jane Sorogo amesema Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano inaratibu ajira nje ya nchi ili kulinda usalama wa watanzania kupitia balozi zetu.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, amesisitiza kuwa mfuko huo ni mkombozi wa sekta binafsi kwani hata waliopo sekta binafsi wanaweza kuweka akiba na kunufaika na mafao ya hifadhi ya jamii ambapo amehamasisha vijana hao kujiunga na kujiwekea akiba kwa ajili ya kesho bora.