Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za uendeshaji wa Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo kutoka Idara ya Mafunzo ya Kilimo na Utafiti, Godfrey Moshi.

Loraine Ronchi Kiongozi wa Kimataifa wa Benki ya Dunia anayesimamia masuala ya kuongeza na kusambaza maarifa na ubunifu katika sekta ya chakula na biashara ya kilimo (Agribusiness)

………….. 

Na Woinde Shizza, Arusha

Wataalamu wa sekta ya kilimo wameeleza kuwa tafiti za kilimo zina nafasi muhimu katika kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa, huku wakisisitiza umuhimu wa kuhakikisha matokeo ya tafiti yanawafikia wakulima na kutumika kutatua changamoto zinazowakabili.

Kauli hiyo imetolewa katika mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za utafiti za ndani na nje ya nchi, ikiwemo kutoka Swaziland, kwa lengo la kujadili namna ya kuimarisha matumizi ya matokeo ya tafiti kwa manufaa ya jamii.

Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za uendeshaji wa Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo kutoka Idara ya Mafunzo ya Kilimo na Utafiti, Godfrey Moshi, alisema Serikali inaendelea kuwekeza katika tafiti na ubunifu ili kuongeza tija katika sekta ya kilimo.

Alisema pamoja na uwepo wa tafiti nyingi zinazotoa majibu ya changamoto mbalimbali za uzalishaji, bado kuna haja ya kuimarisha mifumo ya kusambaza matokeo hayo kwa walengwa ili yaweze kutumika kwa ufanisi mashambani.

“Tafiti nyingi zimefanyika na kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima, Kipaumbele sasa ni kuhakikisha matokeo hayo yanawafikia walengwa kwa wakati na kwa lugha rahisi inayowawezesha kuyatumia katika shughuli zao za kila siku,” alisema Moshi.

Aliongeza kuwa sekta binafsi inapaswa kushiriki kikamilifu katika kufadhili tafiti na kuhamasisha matumizi ya teknolojia zinazotokana na utafiti ili kuongeza tija, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuboresha masoko ya mazao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk. Thomas Bwana, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya watafiti, sekta binafsi na wakulima ili kuhakikisha matokeo ya tafiti yanatumika kikamilifu katika kuongeza uzalishaji na kuleta maendeleo ya kiuchumi.

Alisema ili Tanzania ifikie malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, ni lazima kuwe na uwekezaji zaidi katika tafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia za kisasa zinazoweza kuongeza ufanisi katika sekta mbalimbali za uzalishaji.

Dk. Bwana alisema changamoto iliyopo si ukosefu wa tafiti, bali ni kiwango kidogo cha matumizi ya matokeo yake kutokana na kukosekana kwa muunganiko wa kutosha kati ya watafiti na watumiaji wa teknolojia hizo.

“Tunapaswa kujenga mazingira yatakayowezesha matokeo ya tafiti kufika kwa walengwa na kutumika kwa vitendo. Ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za utafiti, sekta binafsi na wakulima ni muhimu katika kufanikisha hilo,” alisema.

Washiriki wa mkutano huo walieleza kuwa matumizi ya teknolojia yanayotokana na tafiti yana mchango mkubwa katika kuongeza tija ya uzalishaji, hasa katika sekta ya kilimo, na yanaweza kusaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima huku yakiongeza ushindani wa bidhaa katika masoko.

Walisisitiza kuwa mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yatategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa nchi kutumia maarifa, ubunifu na matokeo ya tafiti katika kuimarisha uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.

Mkutano huo umeelezwa kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika kuijenga Tanzania yenye sekta ya kilimo yenye ushindani, tija na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa.