Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, kwa niaba ya Serikali ameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kumtambua na kumwezesha kijana mwenye ulemavu, Joseph, kuonesha uwezo wake wa kipekee katika matumizi ya teknolojia, sambamba na kuelekeza apatiwe ajira ya kudumu.
Prof. Shemdoe alitoa pongezi na maelekezo hayo Juni 23, 2026 jijini Dodoma, kwa niaba ya Serikali alipokuwa amemuwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026.
Awali alipokuwa akitembelea mabanda ya maonesho, Prof. Shemdoe alipata nafasi ya kutembelea banda la VETA na kukutana na Joseph, kijana asiye na mikono lakini anayetumia miguu yake kuendesha kompyuta, kubuni majengo, samani na kufanya kazi mbalimbali za ubunifu wa kidigitali.
Ameeleza kuvutiwa na uwezo wa kijana huyo na kuipongeza VETA kwa kumpa nafasi ya kuonesha na kuendeleza kipaji chake.
Aidha, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imepata tuzo ya mshindi wa tatu kutokana na ushiriki wake bora katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026, kufuatia mafanikio yake katika kuonesha ubunifu na utoaji wa mafunzo yanayolenga makundi mbalimbali ya jamii.
Pia amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha Joseph anapatiwa ufadhili wa masomo ili kuendelea kukuza ujuzi wake.
Kwa upande mwingine, Prof. Shemdoe ameielekeza Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia Katibu Mkuu wake, Bw. Juma Mkomi, kuhakikisha Joseph anapatiwa ajira ya kudumu kutokana na uwezo mkubwa aliouonesha.

