Katika kipindi ambacho mataifa duniani yanaingia katika ushindani mkubwa wa kiuchumi, teknolojia na ushawishi wa kidiplomasia, Tanzania nayo inaonekana kuanza kufanya Diplomasia yake kimkakati katika jukwaa la kimataifa. Ziara ya Kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Urusi, imekuja katika wakati ambao dunia inatafuta washirika wapya wa kiuchumi huku mataifa ya Afrika yakizidi kuwa kitovu muhimu cha uwekezaji, biashara na ushawishi wa kisiasa duniani.
Ziara hiyo inayofanyika kwa mwaliko wa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, siyo tu mwendelezo wa historia ya uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Urusi, bali pia ni ishara ya namna Tanzania inavyotafuta kujijenga upya kiuchumi kupitia diplomasia ya uchumi, uwekezaji, teknolojia na ushirikiano wa kimataifa.
Ziara hiyo imebeba uzito mkubwa wa kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia, hasa ikizingatiwa kuwa ni mara ya pili kwa Rais wa Tanzania kufanya ziara rasmi nchini humo tangu ile ya kihistoria ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1969.
Kwa mtazamo wa kiuchambuzi, ziara hii inaonyesha namna Tanzania chini ya Rais Samia ilivyoamua kuipanua zaidi diplomasia yake ya uchumi kwa kufungua milango mipya ya ushirikiano wa kimataifa nje ya washirika wa jadi wa Magharibi. Tanzania inaonekana kujiweka katika nafasi ya kunufaika na ushindani wa nguvu za kiuchumi duniani kwa kujenga uhusiano wenye tija na mataifa makubwa yenye ushawishi wa kisiasa na kiuchumi kama Urusi.
Kisiasa, ziara hii inadhihirisha kuongezeka kwa hadhi ya Tanzania katika medani za kimataifa. Kukutana kwa Rais Samia na Rais Vladimir Putin katika Ikulu ya Kremlin ni ishara ya heshima na umuhimu ambao Urusi inaipa Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki na Bara la Afrika kwa ujumla.
Katika kipindi ambacho dunia inashuhudia mabadiliko makubwa ya kisiasa na kiuchumi, Tanzania inaonekana kuchukua msimamo wa diplomasia ya ushirikiano badala ya kuegemea upande mmoja wa nguvu za dunia. Hii ndiyo siasa ya kimkakati ambayo Tanzania imekuwa ikiijenga tangu enzi za Mwalimu Nyerere ya kuwa rafiki wa mataifa mbalimbali huku ikiangalia maslahi mapana ya taifa.
Kwa upande wa kidiplomasia, ziara hii inaweza kuimarisha zaidi ushawishi wa Tanzania katika majukwaa ya kimataifa. Ushiriki wa Rais Samia katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF 2026) unaipa Tanzania nafasi ya kuzungumza moja kwa moja na viongozi wa serikali, wawekezaji wakubwa, taasisi za fedha na wadau wa maendeleo kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Hii ina maana kuwa Tanzania haitakuwa tena mtazamaji katika mijadala ya uchumi wa dunia, bali mshiriki anayewasilisha agenda zake za maendeleo, hususan Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga uchumi wa viwanda, ajira, uwekezaji, matumizi ya teknolojia na ushindani wa kimataifa.
Kiuchumi, hapa ndipo uzito mkubwa wa ziara hii ulipo. Tanzania inaingia Urusi ikiwa na ajenda mahsusi ya kutafuta mitaji, teknolojia, masoko na uwekezaji utakaosaidia kukuza uchumi wa ndani. Sekta zilizowekwa mbele katika mazungumzo kati ya Tanzania na Urusi zinaonyesha wazi maeneo ambayo Tanzania inataka kuyatumia kama injini ya uchumi wake mpya.
Katika sekta ya nishati na madini, Urusi ni moja ya mataifa yenye teknolojia kubwa duniani. Ushirikiano katika eneo hili unaweza kuisaidia Tanzania kuongeza thamani ya rasilimali zake, kuimarisha utafiti wa madini na kukuza matumizi ya teknolojia katika uzalishaji.
Katika elimu, sayansi na teknolojia, Tanzania inaweza kunufaika kwa kupata wataalamu, mafunzo pamoja na ushirikiano wa vyuo vikuu na taasisi za tafiti. Kwa miaka mingi, Urusi imekuwa mmoja wa washirika muhimu wa Tanzania katika kuzalisha wataalamu wa kada mbalimbali wakiwemo madaktari, wahandisi, wataalamu wa sayansi, teknolojia, kilimo, anga pamoja na sekta za ulinzi na nishati. Tangu enzi za Muungano wa Kisovieti, wanafunzi wengi wa Kitanzania walipelekwa kusoma nchini Urusi kupitia ufadhili na programu za ushirikiano wa kielimu, jambo lililosaidia Tanzania kupata wataalamu waliokuja kuwa sehemu muhimu ya ujenzi wa taifa. Hii ndiyo sababu ushirikiano wa elimu unaendelea kuonekana kuwa eneo la kimkakati katika mahusiano ya nchi hizi mbili.
Hii ndiyo sababu ziara hii imebebwa pia na agenda ya kujenga rasilimali watu, jambo ambalo linaonekana kupewa uzito mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya ukuaji wa uchumi usiozalisha ajira za kutosha kwa vijana. Kupitia ushirikiano wa kiteknolojia na uwekezaji wa viwanda, serikali inaonekana kutafuta suluhisho la muda mrefu la kuongeza uzalishaji, kukuza viwanda na kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la dunia.
Pia ushiriki wa Rais Samia katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi unaonyesha dhamira ya kuongeza kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili ambacho kwa sasa bado ni kidogo ukilinganisha na ukubwa wa uchumi wa mataifa hayo.
Ikiwa Tanzania itaweza kuvutia wawekezaji kutoka Urusi katika maeneo ya kilimo, mbolea, nishati, madini, utalii, usafirishaji na teknolojia ya habari, kuna uwezekano mkubwa wa kuona ongezeko la ajira, mapato ya ndani pamoja na uhamishaji wa teknolojia.
Lakini pia ziara hii ina ujumbe mkubwa wa kisiasa kimataifa. Katika kipindi ambacho Urusi imekuwa ikitafuta kuimarisha ushawishi wake barani Afrika, Tanzania inaonekana kutumia nafasi hiyo kujinufaisha kiuchumi bila kuingia katika migogoro ya kisiasa ya mataifa makubwa duniani.
Huu ni mwendelezo wa sera ya Tanzania ya kutanguliza maslahi ya taifa katika diplomasia ya kimataifa. Serikali ya Rais Samia inaonekana kuamini kuwa katika dunia ya sasa, mafanikio ya nchi hayatategemea tu siasa nzuri, bali uwezo wa taifa kujenga mtandao mpana wa washirika wa maendeleo na uwekezaji.
Kutunukiwa kwa Rais Samia Shahada ya Heshima ya Uzamivu na Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Urusi (RUDN University) pia ni ishara ya namna uongozi wake unavyoendelea kutambulika kimataifa. Hii inaongeza hadhi ya Tanzania katika diplomasia ya elimu, utalii na ushirikiano wa kimataifa.
Kwa ujumla, Watanzania wanapaswa kuitazama ziara hii kama sehemu ya mkakati mpana wa kuibadilisha Tanzania kiuchumi kupitia diplomasia ya uchumi, uwekezaji, teknolojia na ushirikiano wa kimataifa. Matokeo yake yanaweza yasionekane mara moja, lakini msingi unaowekwa sasa unaweza kuwa muhimu katika kuamua mwelekeo wa uchumi wa Tanzania katika miaka ijayo.
Ziara ya Rais Samia nchini Urusi inaweza kuwa mwanzo wa awamu mpya ya ushirikiano wa kimkakati unaounganisha historia ya muda mrefu ya Tanzania na Urusi na mahitaji mapya ya maendeleo ya Tanzania ya karne ya 21.
