Na. Meleka Kulwa, Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma 

Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imeendelea kuimarisha uwezeshaji wa wafanyabiashara ndogondogo nchini ambapo zaidi ya wafanyabiashara 8,400 wamenufaika na mikopo yenye masharti nafuu yenye thamani ya Shilingi bilioni 17.9.Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027, leo Juni 1 , 2026 bungeni jijini Dodoma Waziri Dkt. Dorothy Gwajima amesema hadi Aprili 2026 jumla ya wafanyabiashara ndogondogo 8,426 wamekopeshwa fedha hizo kupitia mpango maalum unaotekelezwa kwa kushirikiana na Benki ya NMB.

Amebainisha Kuwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, wizara ilipokea Shilingi bilioni 10.5 kwa ajili ya utoaji wa mikopo hiyo, na kufanya kiasi kilichopokelewa tangu kuanza kwa mpango huo Januari 2025 kufikia Shilingi bilioni 18.5.Mbali na mikopo, wizara imeendelea na zoezi la kuwatambua na kuwasajili wafanyabiashara ndogondogo kupitia mfumo wa kidijitali.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, jumla ya wafanyabiashara ndogondogo 143,053 wamejisajili tangu kuanza kwa zoezi hilo mwaka 2024, huku zaidi ya 51,000 wakipatiwa vitambulisho vyao vya kidijitali.

Dkt. Gwajima amesema hatua hiyo inalenga kuwarasimisha wafanyabiashara hao, kuwawezesha kupata huduma za kifedha na kuongeza mchango wao katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya biashara na uwezeshaji wa makundi maalum ili kuchochea maendeleo ya wananchi na kuongeza ajira nchini.