Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imetangaza vipaumbele saba itakavyovitekeleza katika mwaka wa fedha 2026/27 kwa lengo la kujenga jamii imara, jumuishi na yenye maendeleo endelevu.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027, leo Juni 1 , 2026 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amesema wizara hiyo itajikita katika maeneo yenye matokeo makubwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kipaumbele cha kwanza ni kujenga mtaji watu wa Taifa na kizazi cha Tanzania ya mwaka 2050 kinachozingatia maadili, uzalendo, haki, usawa na maendeleo jumuishi.
Amebainisha kipaumbele kingine ni kuimarisha huduma za ustawi wa jamii, malezi na makuzi ya watoto pamoja na mifumo ya ulinzi wa kijamii ili kuendelea kujenga Taifa lenye mshikamano na utu wa kibinadamu.
Vilevile, wizara itaimarisha mifumo ya uwezeshaji wanawake, kukuza usawa wa kijinsia na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika shughuli za maendeleo.
Katika eneo la uchumi, wizara imepanga kufanya mageuzi ya uchumi wa makundi maalum na sekta isiyo rasmi kwa kuyawezesha makundi hayo kuhamia katika uchumi rasmi wenye tija na ushindani.
Pia, wizara itaimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali na takwimu katika utoaji wa huduma za kijamii pamoja na kufanya maamuzi yanayotegemea ushahidi wa kitakwimu.
Kipaumbele kingine ni kujenga jamii yenye amani, uwajibikaji na mshikamano huku ikiongeza ushirikiano wa kimkakati kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za dini, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo.
Dkt. Gwajima alisema utekelezaji wa vipaumbele hivyo utakuwa msingi wa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
