Na Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umeendelea kuandika historia katika kuimarisha huduma za mawasiliano nchini kwa kutekeleza miradi mbalimbali iliyobadili maisha ya mamilioni ya Watanzania, hususan wanaoishi ya vijijini na yasiyo na mvuto wa kibiashara kwa kampuni za mawasiliano.
Kupitia utekelezaji wa miradi hiyo, UCSAF imefanikiwa kusogeza huduma za mawasiliano karibu zaidi na wananchi, hatua inayochochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali, kuboresha upatikanaji huduma za kijamii na kuongeza fursa za maendeleo nchini.
Hadi kufikia Aprili 2026, Serikali kupitia UCSAF imeingia makubaliano ya kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 2,293 zenye vijiji 5,489 na wakazi zaidi ya milioni 32.5. Kati ya maeneo hayo, kata 1,979 zenye vijiji 5,074 tayari zinapata huduma za mawasiliano kupitia minara 2,151 iliyojengwa, huku utekelezaji ukiendelea katika maeneo mengine.
Mafanikio makubwa yameonekana kupitia mradi wa ujenzi wa minara 758 uliokamilika na kunufaisha wananchi zaidi ya milioni 8.5. Mradi huo ulizinduliwa rasmi Aprili 10, 2026 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mbali na ujenzi wa minara mipya, UCSAF imeboresha minara 304 kutoka teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G, hatua iliyoongeza upatikanaji wa intaneti yenye kasi na huduma za kidijitali katika maeneo mengi ya vijijini.
Aidha, utekelezaji wa awamu ya kumi ya mradi wa kufikisha mawasiliano vijijini unaendelea ambapo minara 287 inajengwa katika kata 287 zenye wakazi karibu milioni tatu. Serikali pia imeanza maandalizi ya awamu ya kumi na moja itakayohusisha ujenzi wa minara 280 katika maeneo ya kimkakati ikiwemo reli ya kisasa ya SGR, reli ya TAZARA, maeneo ya mipakani na hifadhi za taifa.
Katika sekta ya utangazaji, UCSAF imefanikisha ujenzi wa vituo 11 vya kurushia matangazo ya Redio ya Taifa (TBC) na inaendelea na ujenzi wa vituo vingine 21. Vilevile, imeendelea kuimarisha redio za jamii kupitia ujenzi wa studio, minara ya matangazo na ununuzi wa vifaa vya kisasa.
Sekta ya elimu nayo imeendelea kunufaika ambapo shule za umma 1,121 zimepatiwa vifaa vya TEHAMA na maabara za kompyuta. UCSAF pia imewezesha shule 22 zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa kuwapatia vifaa vya kisasa vya kujifunzia, huku shule nyingine 10 zikitarajiwa kunufaika katika mwaka wa fedha 2025/26.
Katika kuimarisha matumizi ya teknolojia mashuleni, walimu 3,808 wa shule za msingi na sekondari wamepatiwa mafunzo ya TEHAMA tangu kuanzishwa kwa mpango huo. Wasichana zaidi ya 1,300 pia wamefikiwa kupitia programu ya Girls in ICT inayolenga kuwahamasisha kushiriki katika masomo na taaluma za teknolojia.
UCSAF pia inaendelea kutekeleza mradi wa huduma za bure za intaneti katika maeneo mbalimbali ya umma nchini. Vituo vya huduma hiyo vimeanzishwa katika maeneo kadhaa ikiwemo Dodoma, Mwanza, Zanzibar, Tabora na Dar es Salaam, huku utekelezaji ukiendelea katika maeneo mengine 60 Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza katika mkutano maalum na wahariri wa vyombo vya habari Mkoa wa Dodoma uliofanyika Mei 15, 2026, Kaimu Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Albert Richard, alisema ushirikiano kati ya UCSAF na vyombo vya habari ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.
Kwa upande wa wananchi, mafanikio ya miradi hiyo yanaonekana wazi katika maisha yao ya kila siku. Mkazi wa Kijiji cha Ngaraseo, Alen Molei, alisema kabla ya ujio wa minara ya UCSAF walikabiliwa na changamoto kubwa ya mawasiliano na wakati mwingine walilazimika kutumia mitandao ya nchi jirani au kutegemea minara ya vijiji vya mbali.
Alieleza kuwa hali hiyo imebadilika kwa sasa kwani wananchi wanapata mawasiliano kwa urahisi, huduma za afya zimekuwa karibu zaidi kupitia mawasiliano ya haraka, na shughuli za kiuchumi zimeimarika kwa kiasi kikubwa.
Wananchi wengine wameishukuru UCSAF kwa kuwasogezea huduma za mawasiliano karibu na makazi yao, jambo lililorahisisha miamala ya kifedha, biashara na mawasiliano na ndugu walioko mbali.
Naye Petro Nasi, mkazi wa Kijiji cha Endo, alisema kabla ya kujengwa kwa mnara wa mawasiliano wananchi walilazimika kupanda milimani kutafuta mtandao, lakini sasa huduma zinapatikana kwa urahisi ndani ya kijiji.
Kwa ujumla, UCSAF inaendelea kuwa mhimili muhimu wa utekelezaji wa Dira ya Tanzania ya Kidijitali kwa kuhakikisha huduma za mawasiliano, intaneti na TEHAMA zinawafikia wananchi wote bila kujali mahali wanapoishi.

