NA DENIS MLOWE, IRINGA
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa na kamati ya kudumu ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo wamekoshwa na kiwango cha uwekezaji uliofanywa kwenye sekta ya Maziwa mkoani Iringa.
Akizungumza mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea na kukagua shughuli za ufugaji na uzalishaji maziwa kwenye kiwanda cha ASAS, Balozi Dkt. Bashiru amewataka wafugaji kuheshimu misingi ya sayansi na taaluma ili wawe na ufugaji wenye ufanisi na wa kibiashara.
“Tumeona wataalam ambao amewaajiri ASAS wanaelewa kazi yao na katika hili nchi imefundisha sana wataalam hivyo ni lazima tuheshimu utaalam wao lakini pia tuwape nafasi na nyenzo za kuonesha utaalam wao” Amesisitiza Balozi Dkt. Bashiru.
Aidha Balozi Dkt. Bashiru amempongeza mwekezaji huyo kwa kuweka miundombinu bora ya uvunaji wa maji ya mvua na matumizi bora ya ardhi kwa upande wa uzalishaji wa malisho ya mifugo ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ambayo yamekuwa yakitolewa na Serikali kwa wafugaji ili kuwa na uhakika wa chakula na maji ya kunyweshea mifugo yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo Mhe. Deodatus Mwanyika amesema kuwa uwekezaji huo umeipa nguvu kamati hiyo ya kuishauri Serikali juu ya njia bora za kuendeleza sekta hiyo ya maziwa.
“Huu ndo uwekezaji ambao Watanzania tunautegemea kwa sababu tuna ardhi kama nchi lakini sidhani kama tumeitumia kama ambavyo ASAS wanaitumia, yaan kama tungekuwa na kampuni hata 10 tu kama hii tungekuwa mbali sana” Ameongeza Mhe. Mwanyika.
Naye Mkurugenzi wa kiwanda hicho Bw. Fuad Jaffer mbali na kuishukuru Serikali kwa ushirikiano mkubwa anaopewa ameongeza mbali na kuzalisha maziwa mkakati mwingine wa shamba hilo ni kuzalisha mitamba ili kuwasaidia wafugaji wengine wanaohitaji mbegu bora za ng’ombe wa maziwa.
Ziara hiyo iliendelea katika shamba la Mifugo na kiwanda cha kusindika maziwa cha Shafa huku kivutio kingine kwa viongozi hao kikiwa ni Shamba la mwekezaji Richard Philips maarufu kama Kibebe ambaye aliishukuru Serikali kwa kuwapatia chanjo ya ugonjwa wa homa ya mapafu ya ng’ombe.

