Na Hassan Kimweri, WAF – Kagera
Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe amewataka watumishi wa afya nchini kuwa makini zaidi katika kipindi hiki cha tahadhari ya ugonjwa wa Ebola, kufuatia mlipuko uliojitokeza katika nchi jirani za Congo na Uganda ili kujikinga wao na kuwakinga wengine.
Dkt. Magembe amesema hayo leo Mei 31, 2026 wakati akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera na Hospitali ya Manispaa ya Bukoba akihitimisha ziara yake ya kukagua hali ya utayari wa kujikinga na ugonjwa wa ebola usiingie nchini katika maeneo ya mipakani mkoani humo.
Dkt. Magembe amesema kuwa dalili za awali za Ebola kama homa, kuumwa kichwa, uchovu wa mwili, kutapika na kuharisha zinaweza kufanana na magonjwa mengine, hivyo wahudumu wa afya wanapaswa kuwa na umakini mkubwa wanapowahudumia wagonjwa na kuchukua tahadhari zote muhimu za kinga.
“Tumieni vifaa kinga binafsi (Personal Protective Gears) ikiwemo barakoa, gloves, apron, kofia, miwani ya kinga na vifaa vingine vinavyotakiwa kulingana na mazingira ya kazi”, amesema Dr Magembe
“Chukueni historia sahihi za wagonjwa, ikiwemo kuwauliza kuhusu dalili za Ebola na historia ya safari katika maeneo yaliyoathirika, hususan Congo na Uganda, ili kusaidia utambuzi wa mapema wa ugonjwa huo,” amesema Dkt. Magembe
Dkt. Magembe alihimiza watumishi wa afya kuendelea kufuata taratibu zote za kitaalamu za uchukuaji wa sampuli, matumizi ya vifaa tiba na utupaji wa taka za hospitali, akisisitiza kuwa kujikinga binafsi ni njia bora ya kuwalinda wagonjwa, wafanyakazi wengine na jamii kwa ujumla.

