WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba ameagiza kukamatwa kwa mtumishi mwingine wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni anayedaiwa kuhusika katika mtandao wa kulinda na kutetea watumishi waliohusishwa na ubadhirifu wa zaidi ya shilingi milioni 500, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwafuatilia wote waliohusika na wizi wa fedha za umma.
“Mkuu wa mkoa, mtume wa RPC, huyu naye akamatwe, aunganishwe. Nataka mtandao huu wa mchwa nitimue wote. Sina urafiki wala uungwana na wezi, walaghai, wazembe na wanyang’anyi,” amesema Dkt. Mwigulu.
Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo leo Jumapili Mei 31, 2026 alipokuwa akizungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake katika eneo la Madukani, wilayani Ikungi mkoani Singida.
Amesema amepokea taarifa kuwa mmoja wa watumishi wa Halmashauri ya Manyoni amekuwa akipinga hatua zilizochukuliwa dhidi ya watumishi waliohusishwa na ubadhirifu huo, ikiwemo kutajwa kwa majina yao hadharani, jambo ambalo amesema linaashiria kuwepo kwa mtandao unaolenga kuwalinda wahusika.
“Eti analalamika kwa nini nimewataja kwa majina. Anataka tuwatunzie heshima wezi. Mwizi hatakiwi kufichwa wala kulindwa. Akamatwe na hatua zichukuliwe mara moja,” amesema.
Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa Serikali haitaridhia utamaduni wa kuwahamisha watumishi wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu badala ya kuwawajibisha, akieleza kuwa hatua za kisheria, kinidhamu na urejeshaji wa fedha za wananchi lazima zitekelezwe kikamilifu.
“Hakuna kuhamisha mwizi. Akihamishwa anaenda kuiba sehemu nyingine. Wale wote waliohusika wakamatwe, warejeshe fedha za wananchi na hatua za kisheria zifuate,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amesema ataendelea kusimamia matumizi ya fedha za umma katika halmashauri zote nchini ili kuhakikisha fedha zinazokusanywa kutoka kwa walipa kodi zinatumika kwa maendeleo yaliyokusudiwa.
“Nitashughulika na mchwa wanaokula fedha kwenye halmashauri zetu. Tunataka fedha za wananchi zitumike kujenga shule, vituo vya afya, barabara na miradi mingine ya maendeleo, si kugawanywa na wachache,” amesema.
Sambamba na hilo, amekemea vitendo vya ubadhirifu katika sekta ya afya ambapo wananchi huagizwa kununua dawa katika maduka binafsi licha ya Serikali kupeleka fedha za ununuzi wa dawa katika vituo vya kutolea huduma.
“Haiwezekani Serikali ipeleke fedha za dawa halafu wananchi waambiwe wakazinue dawa mtaani. Hii ni michezo ambayo haitavumiliwa,” amesema.
Waziri Mkuu pia amewahakikishia wananchi wa Ikungi kuwa atarejea wilayani humo mwezi Juni mwaka huu kwa ziara maalum ya kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
“Nitakuja mwezi huu wa sita kabla haujaisha. Tutakaa siku nzima, tusikilizane na kutatua kero za wananchi,” amesema.

