Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe ambaye halimashauri za wilaya Majiji na miji zimo kwake na huko ndiko kwenye wajasiriamali wenyewe.
…………….
Katika kipindi hiki ambapo vijana wengi nchini wanaingia kwenye shughuli za ujasiriamali, biashara ndogo ndogo pamoja na huduma mbalimbali za kujiajiri, bado ipo haja kubwa ya kuongeza elimu ya msingi kuhusu namna sahihi ya kuanzisha na kuendesha biashara.
Wakati vijana wengi wanakuwa na hamasa ya kutafuta mitaji na kuanzisha biashara, bado sehemu kubwa yao hukosa maarifa muhimu kuhusu usajili wa biashara, ulipaji kodi, leseni, utunzaji wa kumbukumbu za fedha pamoja na sheria na taratibu zinazohitajika kabla ya biashara kuanza rasmi.
Kutokana na hali hiyo, ipo haja kwa taasisi za fedha kushirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) pamoja na mamlaka za majiji, manispaa na halmashauri za miji ili kuanzisha mkakati maalum wa pamoja wa kutoa elimu kwa vijana kuhusu mambo muhimu kabla ya kuanzisha biashara.
Theobald Sabi Mwenyekiti wa Chama cha Taasisi za Benki (TBA)
Kwa miaka mingi, taasisi mbalimbali zimekuwa zikitoa elimu kupitia maonesho ya biashara, wiki za huduma kwa wananchi na matukio mbalimbali ya kitaasisi. Hata hivyo, mfumo huo umekuwa ukiwafikia zaidi watu ambao tayari wamejipanga kuhudhuria maonesho hayo kwa lengo maalum la kutafuta taarifa au huduma fulani.
Matokeo yake, bado vijana wengi waliopo mitaani, wanaoanza biashara kwa mazingira ya kawaida au wanaofanya shughuli za ujasiriamali kwa kujifunza wenyewe, wameendelea kubaki nje ya mfumo rasmi wa elimu hiyo muhimu.
Ndiyo maana ipo haja ya kutoka kwenye mtindo wa kila taasisi kwenda kivyake kwenye maonesho na badala yake kuanzishwa kwa mfumo wa pamoja wenye nguvu zaidi wa kuwafikia vijana moja kwa moja kupitia makongamano, mikutano ya wazi, semina maalum za biashara pamoja na programu za elimu zinazowakusanya vijana wengi kwa wakati mmoja.
Mfumo huo ukiwa wa pamoja unaweza kutoa ujumbe wenye nguvu na kujenga uelewa mpana zaidi kwa vijana kuliko pale kila taasisi inapotoa elimu kivyake. Vijana wanapokutana sehemu moja na kupata maelezo kutoka kwa taasisi zote muhimu kwa wakati mmoja, huwa rahisi kuelewa uhusiano wa huduma hizo katika safari ya biashara zao.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Yusuph Mwenda
Kwa mfano, kijana anaweza kuelezwa kwa wakati mmoja umuhimu wa kusajili biashara kupitia BRELA, kupata TIN na kuelewa masuala ya kodi kupitia TRA, kujua taratibu za leseni kutoka halmashauri pamoja na namna ya kupata na kutumia mikopo vizuri kutoka taasisi za fedha.
Elimu ya pamoja ya aina hiyo inaweza kuwasaidia vijana kuona biashara kama mfumo kamili unaohitaji maandalizi, nidhamu na uelewa wa hatua zote muhimu badala ya kuangalia mtaji pekee.
Aidha, Serikali inaweza kwenda hatua zaidi kwa kuunda kikosi kazi maalum au task force kitakachojumuisha taasisi hizo zote kwa lengo la kuratibu kampeni za kitaifa za elimu ya biashara kwa vijana. Task force hiyo inaweza kufanya kazi chini ya uratibu wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI ili kuhakikisha elimu hiyo inafika kwa vijana katika ngazi zote kuanzia mikoa, majiji, manispaa, halmashauri hadi ngazi za kata na mitaa.

Godfrey Nyaisa kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela)
Kupitia uratibu huo wa TAMISEMI, kikosi kazi hicho kinaweza kufanya ziara kwenye vyuo, maeneo ya biashara, vikundi vya vijana, masoko pamoja na kutumia majukwaa ya kidigitali kuwafikia vijana wengi zaidi waliopo mijini na vijijini. Mfumo huo unaweza kusaidia pia kuweka mwendelezo wa elimu badala ya kuwa matukio ya muda mfupi yanayofanyika mara moja moja.
Faida kubwa ya taasisi hizi kuwa pamoja ni kujenga umakini mkubwa kwa vijana.
Mara nyingi taasisi zinapotoa elimu kila moja kivyake, vijana hupata taarifa kwa vipande vipande na wakati mwingine hukosa mwendelezo wa kile wanachotakiwa kufanya. Lakini wakipewa elimu kwa mfumo mmoja uliounganishwa, huwa rahisi kuona picha kamili ya safari ya biashara kuanzia hatua ya wazo hadi biashara kuwa rasmi na endelevu.
Vilevile, mfumo huo unaweza kusaidia kupunguza changamoto za biashara kufungwa mapema, migogoro ya kodi, biashara zisizosajiliwa pamoja na matumizi mabaya ya mikopo kutokana na ukosefu wa elimu sahihi.
Katika mazingira ya sasa ambapo vijana wengi wanajihusisha na biashara za mtandaoni, ubunifu wa huduma, sanaa, kilimo biashara na shughuli mbalimbali za ujasiriamali, elimu sahihi inaweza kuwa silaha muhimu ya kuwasaidia kujenga biashara zenye mafanikio na zinazodumu kwa muda mrefu.
Kwa ujumla, ushirikiano wa taasisi za fedha, TRA, BRELA pamoja na mamlaka za serikali za mitaa unaweza kuwa mwanzo mzuri wa mapinduzi ya elimu ya biashara kwa vijana nchini. Endapo mkakati huo utawekwa kwa mfumo wa pamoja, wenye uratibu na unaowafikia vijana moja kwa moja, unaweza kuzaa matunda makubwa ya kiuchumi na kusaidia kujenga kizazi cha vijana wenye biashara rasmi, endelevu na zenye mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa.
