Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu, akizungumza jambo na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), baada ya kumalizika kwa kikao cha kujadili agenda zinazohusu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano Mkuu wa 61 wa mwaka 2026 wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na Mkutano Mkuu wa 52 wa Mwaka wa Mfuko wa Maendeleo wa Benki hiyo (ADF),ambapo Mhe. Balozi Omar aliwasilisha taarifa hiyo. Mikutano hiyo itakaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kintélé, Congo, Brazaville.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Hamad Omar Bakar (Mb), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali ambaye pia katika Muundo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika ni Gavana Mbadala wa Benki hiyo (Alternate Governor), Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Kaimu Naibu Katibu Mkuu ambaye pia ni Kamishna wa Fedha za Nje, Bw. Rished Bade, Viongozi wengine kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Zaidi ya wajumbe 3,000 kutoka nchi mbalimbali za Afrika na Kimataifa, wanatarajiwa kuhudhuria Mkutano Mkuu huo, Utakaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kintélé, wakiwemo Marais na Wakuu wa Serikali za Afrika, Mawaziri wa Fedha, Magavana wa Mabenki Kuu, washirika wa maendeleo, wawakilishi wa sekta binafsi, viongozi wa asasi za kiraia, wasomi, taasisi za utafiti, NGOs, na wadau wengine.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Kuhamasisha Ufadhili wa Maendeleo ya Afrika kwa Wingi katika Dunia Iliyogawanyika”. Kauli hii inasisitiza umuhimu wa kuziba pengo la kifedha linalokua kwa mahitaji ya maendeleo ya Afrika, hasa katika mazingira ya kisiasa na kiuchumi duniani yanayobadilika kwa kasi.